Southampton yaipa Man City kichapo cha 8 msimu huu
Na CHRIS ADUNGO
CHE Adams, 23, alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Southampton dhidi ya Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 5, 2020 uwanjani St Mary’s.
Adams ambaye alisajiliwa na Southampton kutoka Birmingham City kwa kima cha Sh2.1 bilioni mnamo Julai 2019, alivurumisha kombora kutoka hatua ya 40 baada ya kumzidi maarifa kiungo Oleksandr Zinchenko na kumwacha hoi kipa Ederson Moraes.
Kocha Pep Guardiola alikifanyia kikosi chake cha Man-City kilichowapepeta Liverpool 4-0 katika gozi la Julai 2, 2020 uwanjani Etihad jumla ya mabadiliko sita. Kati ya masogora wa haiba kubwa waliopumzishwa na Guardiola ni kiungo Kevin de Bruyne anayepigiwa upatu wa kutawazwa Mchezaji Bora zaidi wa EPL msimu huu.
Bao la Southampton liliamsha hasira za Man-City ambao walikita kambi langoni pa wenyeji wao kwa kipindi kirefu. Hata hivyo, kipa Alex McCarthy alisalia imara na akapangua makombora makali aliyoelekezewa na Fernandinho, Raheem Sterling, Gabriel Jesus na David Silva.
Ingawa Southampton pia walipata nafasi kadhaa za wazi, fursa hizo zilipotezwa na washambuliaji Nathan Redmond, Danny Ings na Stuart Armstrong.
Southampton walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo wakilenga kutorudia makosa yaliyowashuhudia Man-City wakitoka nyuma na kusajili ushindi wa 2-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Novemba 2019 uwanjani Etihad.
Matokeo yaliyosajiliwa na Man-City ugani St Mary’s yaliwasaza masogora wa Guardiola katika nafasi ya pili jedwalini huku pengo la alama 23 likitamalaki kati yao na Liverpool waliowacharaza Aston Villa 2-0 na kufikisha pointi 89 katika mechi nyingine ya Julai 5, 2020.
Zikisalia mechi tano zaidi msimu huu, Southampton kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 baada ya kuvuna alama 43 kutokana na mechi 33 chini ya mkufunzi Ralph Hasenhuttl. Ushindi dhidi ya Man-City ulihakikisha kwamba wanajizolea jumla ya alama 17 kutokana na mechi 17 za nyumbani hadi kufikia sasa msimu huu.