Spurs wamwachilia Ryan Sessegnon ajiunge na Hoffenheim ya Ujerumani kwa mkopo
Na MASHIRIKA
KIUNGO Ryan Sessegnon wa Tottenham Hotspur amejiunga na kikosi cha Hoffenheim nchini Ujerumani kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Sogora huyo mwenye umri wa miaka 20 aliwahi kuchezea Fulham kama beki wa kushoto na wing’a kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Spurs kwa kima cha Sh3.5 bilioni mnamo Agosti 2019.
Hata hivyo, alishindwa kuhimili viwango vya ushindani mkali kambini mwa Tottenham na akajipata akisugua benchi mara kadhaa. Nyota huyo ambaye hajawajibishwa katika mchuano wowote wa EPL msimu huu wa 2020-21, alichezeshwa na Spurs mara 12 pekee ligini katika msimu wa 2019-20.
Hoffenheim kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kupiga mechi tatu za ufunguzi wa msimu huu ambao pia utawashuhudia wakinogesha kipute cha Europa League.
Fowadi wa Arsenal, Reiss Nelson ambaye hushirikiana na Sessegnon katika kikosi cha chipukizi wa U-21 nchini Uingereza, aliwahi kuchezea Hoffenheim kwa mkopo mnamo 2018-19. Aliwajibishwa mara 29 na akafunga mabao saba.