• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
St Anthony High na Dagoretti High katika fainali kali

St Anthony High na Dagoretti High katika fainali kali

Na BENSON AYIENDA na JOHN ASHIHUNDU

ST Anthony High School kutoka Rift Valley na Dagoretti High School ya Nairobi zitakutana leo Jumamosi katika fainali ya kuwania ubingwa kitaifa kwa shule za sekondari.

Timu hizo ziliibuka na ushindi dhidi ya Olbolsat ya jimbo la Kati na Ebwali kutoka Magharibi kwenye mechi za nusu-fainali, jana katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na Coca Cola.

Katika nusu-fainali ya kwanza, Dagoretti ambao mwaka uliopita waliondolewa katika hatua ya nusu-fainali mjini Eldoret waliichapa Olbolsat 3-1 na kufuzu.

Timu zote zilikutana baada ya kuandikisha matokeo mema kwenye mechi za makundi huku Dagoretti wakimaliza wa kwanza katika Kundi A kwa pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu wakati Olbolsat wakimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi B kwa pointi sita baada ya kupoteza mechi moja pekee.

Paul Odhiambo aliifungia Dagoretti bao la kwanza dakika ya tatu kabla ya Adan Rashid kusawazishia Olbolsat dakika 12 baadaye.

Baada ya Olbolsat kusawazisha, mechi ilionekana kubadilika huku timu zote zikicheza soka ya kuvutia.

Derick Omondi alimimina wavuni bao la pili na kufanya mambo kuwa 2-1 kufikia wakati wa mapumziko.

Simon Omondi alifunga bao la tatu la Dagoretti kutokana na kombora kali kutoka umbali wa mita 18.

Akizungumza kuhusu mechi hiyo, kocha wa Dagoretti, Joseph Makhoha alisema ushindi wao ulitokana na maandalizi mema, mbali na wachezaji kufuata mawaidha yake.

“Tulikosa kufika fainali za mwaka uliopita, hivyo ikabidi tuzidishe maandalizi yetu. Tuko tayari kwa upinzani wowote fainalini,” alisema.

Huku akikiri upinzani mkali kutoka kwa wapinzani, mwenzake Simon Wakimashia wa kikosi cha Olbolsat alisema timu yake ilijumuisha vijana wengi wa umri mdogo baada ya wengi kuondoka mwaka 2018.

“Kwa sasa tunajitahidi kujenga timu mpya ambayo itachukua muda kukamilika,” alisema.

Katika nusu-fainali ya pili iliyokuwa ngumu ajabu, St Anthony ambao ndio mabingwa wa taji la 2012 waliagana 0:0 na Ebwali Secondary katika muda wa kawaida na wa ziada kabla ya mshindi kuamuliwa kupitia kwa mikwaju ya penalti ambapo St Anthony walishinda kwa 6-5.

Gilbert Ndiema na Kelvin Owalla walishindwa kufunga kwa upande wa Ebwali huku Shamon Ashwar akipoteza kwa upande wa St Anthony.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Ilmuradi una uwezo wa kula vya kuliwa,...

Msimu wa ligi kuu za soka Ulaya watarajiwa kusisimua...

adminleo