Staa wa Starlets amezea mate maisha ya Uturuki
Na CHRIS ADUNGO
LICHA ya kwamba shughuli za michezo zimesitishwa kote duniani kutokana na virusi vya corona, mvamizi Esse Akida wa Harambee Starlets amesisitiza kuwa maazimio yake msimu ujao ni kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) akivalia jezi za kikosi cha Besiktas nchini Uturuki.
Akida, 27, aliingia katika mabuku ya kumbukumbu mnamo 2016 baada ya kufungia Starlets bao la kwanza katika historia ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) dhidi ya Ghana. Hata hivyo, walipokezwa kichapo cha 3-1 katika gozi hilo lililosakatwa nchini Cameroon.
Kenya ilipokezwa baadaye vichapo vya 3-1 na 4-0 kutoka kwa Mali na Nigeria mtawalia na ikivuta mkia katika mashindano hayo ya mataifa manane.
Besiktas walimsajili Akida kutoka klabu ya Hapoel Ramat HaSharon FC ya Israel mnamo Februari 2020. Ili kufuzu kwa kivumbi cha Uefa muhula ujao, Besiktas wana ulazima wa kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uturuki msimu huu. Ufanisi huo utampa Akida jukwaa la kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza mzawa na raia wa Kenya kuwahi kucheza katika soka ya bara Ulaya.
“Kushiriki kipute cha Uefa ndilo jambo kubwa zaidi katika maazimio yangu. Nimejitathmini kwa kina na kutambua kwamba hii ni ndoto ambayo nina uwezo wa kuifikia baada ya corona kudhibitiwa na soka ya Uturuki na Uefa kurejelewa,” akasema Akida katika mahojiano yake na mtandao wa Cafoline.com.
Kufikia jana, Uturuki ilikuwa imeripoti zaidi ya visa 98,500 vya maambukizi ya corona na zaidi ya vifo 2,300 kutokana na janga hilo.
Hadi Ligi Kuu ya Uturuki ilipoahirishwa kwa muda usiojulikana mwanzoni mwa Machi 2020, Akida alikuwa amewajibishwa na Besiktas mara mbili katika kipute hicho ambacho kilikuwa kimefikia raundi ya mechi 15.
Kufikia sasa, Besiktas wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 42 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uturuki (Bayanlar). Ni pengo la pointi moja pekee ndilo linawatenganisha malkia hao wa soka ya Uturuki na viongozi ALG Spor.
Kabla ya kuyoyomea Israel kuchezea FC Ramat, Akisa alikuwa mchezaji wa klabu za Spedag na Thika Queens zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KWPL).
Alipokea malezi yake ya awali kabisa kwenye ulingo wa soka katika klabu ya Moving The Goalposts (MTG) kabla ya kuhemewa na Spedag kisha Thika Queens.
Baada ya kujipatia umaarufu nchini Cameroon mnamo 2016, Akida alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Starlets kilichotegemewa na kocha David Ouma kwenye soka ya COTIF jijini Valencia, Uhispania mwaka uo huo. Aliibuka mchezaji bora zaidi (MVP) katika kivumbi hicho.
Akida alivalia jezi za Starlets kwa mara ya mwisho mnamo 2018 katika fainali za Cecafa zilizoandaliwa jijini Kigali, Rwanda.
Mbali na Akida, Kenya inajivunia wanasoka wengine watatu wa kike wanaosakata soka ya kulipwa ughaibuni. Hao ni pamoja ni Annedy Kundu, Ruth Ingosi (Lakatamia, Cyprus) na Vivian Corazon Odhiambo Aquino wa Atletico Ouriense nchini Ureno.