Starlets imani tele watavuna dhidi ya Ghana
Na CHRIS ADUNGO
VIPUSA wa Harambee Starlets waliondoka humu nchini hapo Jumanne kuelekea jijini Accra, Ghana kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa mchujo wa kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2020.
Akizungumza kabla ya kuondoka, kocha David Ouma alisema kwamba kikubwa zaidi katika maazimio yao ugenini ni kusajili sare au kupata bao litakaloweka hai matumaini yao ya kusonga mbele watakaporejea kwa kivumbi cha marudiano jijini Nairobi mnamo Oktoba 8.
“Maandalizi ambayo tumefanya kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita ni ya kuridhisha. Ninaamini kwamba tutasajili matokeo ya kuridhisha dhidi ya Ghana. Kikosi kinatawaliwa na hamasa tele na kila mmoja yuko tayari kwa kivumbi hiki,” akasema Ouma.
Starlets walikamilisha mazoezi yao uwanjani Camp Toyoyo, Nairobi mnamo Jumatatu huku Ouma akiwachuja wachezaji watatu zaidi kutoka kwa kikosi chake cha awali cha wachezaji 23 aliokuwa nao kambini.
Kwa upande wake, beki Dorcas Shikobe ambaye ni nahodha wa Starlets alisema watapania sana kuepuka kufungwa huku nao wakijitahidi kupata bao muhimu la ugenini. Ouma ataazimia sana kutegemea maarifa ya mshambuliaji Mwanahalima Adam aliyefungia Starlets mabao mawili yaliyowachochea kuwabandua Malawi kwa jumla ya mabao 5-3 katika raundi ya pili mnamo Septemba 1.
“Ghana ni kikosi kizuri sana. Ingawa hivyo, tulifanikiwa kuwalazimishia sare ya 1-1 mnamo 2018. Historia hiyo inatuaminisha zaidi kadri tunavyojiandaa kukizamisha chombo chao,” akasema Adam.
Mshindi baada ya michuano ya mikondo miwili kati ya Kenya na Ghana atafuzu kwa raudi ya nne ya kufuzu ambapo atakutana ama na Zambia au Botswana. Mshindi wa raundi ya nne ataingia raundi ya tano ya kufuzu na atakayetawala hatua hiyo atajikatia tiketi ya kuingia Olimpiki za mwaka ujao. Atakayeshindwa atalazimika kushiriki mchujo mwingine dhidi ya kikosi kitakachoambulia nafasi ya pili kutoka Ukanda wa Soka ya Amerika Kusini (CONMEBOL).