Michezo

Starlets waamini watakung’uta Malawi kampeni ya Olimpiki

July 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Mshambuliaji Mwanahalima Adam amejawa na matumaini Harambee Starlets itaanza vyema kampeni yake ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 itakapolimana na Malawi mwezi ujao.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limeandikia mataifa ya Msumbiji, Zambia, Zimbabwe na Ethiopia barua kuomba mechi za kirafiki dhidi Starlets mapema mwezi Agosti kabla ya kuzuru Malawi mnamo Agosti 26 na kisha kuialika Septemba 1. Linataka Starlets ijipime nguvu mara mbili (mechi moja nyumbani na nyingine ugenini) kabla ya kulimana na Malawi katika raundi ya pili.

Akizungumza katika mazoezi ya timu hiyo ya taifa ya wanawake ya Kenya uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi mnamo Jumatano, mchezaji huyo wa Thika Queens inayoshiriki Ligi Kuu alisema, “Tuko tayari kukutana na Malawi. Niko na matumaini makubwa tutabwaga Malawi.”

Kikosi cha kocha David Ouma cha wachezaji 39 ni mchanganyiko wa wachezaji walio na uzoefu kama Teresa Engesha, Dorcas Shikobe, Corazon Aquino, Adam, Enez Mango, Cynthia Shilwatso na pia wachezaji wapya kama Elizabeth Katungwa, Mercy Airo, Cynthia Matekwa na Wilfrida Seda.

Mchezaji wa Gaspo Youth, Judith Osimbo, ambaye aliibuka kipa bora wa mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom, pamoja na Tumaini Waliaula (Trans Nzoia Falcons), ambaye amefunga zaidi ya mabao 20 ligini, pia wamo mbioni kuchezea Kenya kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Ouma, ambaye aliongoza Harambee Starlets kushiriki Kombe la Afrika la Wanawake (AWCON) kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2016, amesema anaamini kikosi hicho chake.

“Kikosi hiki ni kizuri. Nakiamini,” alisema Ouma na kufichua kuwa Wincate Kaari, Elizabeth Wambui na Winnie Kanyotu watahitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kimatibabu kwa sababu wana majeraha.

Ameongeza kuwa anachoshughulikia wakati huu ni kuimarisha ujuzi wao.

Wachezaji wazoefu kama Neddy Atieno, Wendy Ann Achieng na Cheris Avilia hawamo kikosini.

Kenya ilishuka nafasi tatu hadi nambari 141 kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Julai 12 nayo Malawi inashikilia nafasi ya 146 baada ya kuruka juu nafasi moja.

She-Flames ya Malawi, ambayo inanolewa na kocha Abel Mkandawire, itatumia mashindano ya mataifa ya Afrika ya Kusini (COSAFA) nchini Afrika Kusini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya. Mashindano hayo yatafanyika Julai 31 hadi Agosti 11 mjini Port Elizabeth.

Malawi ilipata tiketi ya kukutana na Kenya katika raundi ya pili baada ya kuchabanga Msumbiji kwa jumla ya mabao 14-1 katika raundi ya kwanza mwezi Aprili. Mshambuliaji Tabitha Chawinga anayesakata soka yake ya malipo nchini Uchina katika klabu ya Jiangsu Suning na mvamizi matata Temwa Chawinga kutoka klabu ya Kvarnsvedens IK nchini Uswidi ni baadhi ya wachezaji matata Kenya italazimika kuwa macho nao itakapokutana na Malawi. Dada hawa walifungia Malawi mabao 10 kati ya 14 ilipata dhidi ya Msumbiji.