Sterling aanzisha vita dhidi ya ubaguzi-rangi
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
MSIMAMO mkali wa mshambuliaji Raheem Sterling wa Manchester City kuhusu ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji wa asili ya Kiafrika unalenga kuwalinda wanasoka wa siku za usoni.
Mwingereza huyo anayewania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa nchini Uingereza (PFA) amekuwa katika mstari wa mbele kupiga vita mwenendo huo wa kuchukiza.
Sterling ambaye ni miongoni mwa waliofanyiwa vitendo hivyo, anaamini kampeni yake kali itapunguza tabia hiyo inayoendeshwa na mashabiki Wazungu.
Majuzi nyota huyo alifokewa vikali na mashabiki wa Chelsea kwenye mechi ambayo walipata ushindi wa 2-0.
“Kwa muda mrefu nimekuwa nikipitia katika hali hii ngumu na singependa kuona wachezaji wengine wakifanyiwa hivyo. Mimi na wenzangu tutajaribu tuwezavyo kupambana na hali hii. Kila mchezaji nimezungmza naye amenihakikishia kuniunga mkono kikamilifu, na sasa tutatafuta mbinu za kubuni sheria kali za kuwaadhibu watu kama hao,” alisema Sterling.
Sterling na Virgil van Dijk wameteuliwa kuwania tuzo ya PFA, lakini amesema halitakuwa muhimu kwake iwapo klabu yake ya Manchester City itakosa kutwa ubingwa wa EPL msimu huu.
“Ninacholenga tu ni kutwaa ubingwa wa EPL na FA Cup, halafu mambo mengine baadaye, ingawa tuzo kama hiyo pia ni muhimu. Mie nilimpigia kura Harry Kane wa Spurs, kwa sababu amekuwa akifunga mabaoi mara kwa mara kabla ya kuumia. Anatoa mchango mkubwa kwa klabu yake. Ni kiongozi mzuri wa timu yetu ya taifa, ni mtu anayejipa heshima. Anakuwa tayari kila mara kusaidia wenzake wanapokuwa na matatizo. Kama mchezaji wa kulipwa, naiga sana mienendo yake, na hiyo ilinifanya nimpigie kura, namsubiri kwa hamu arejee uwanjani,” alisema Sterling.
Sarri ashtakiwa
Kwingineko, kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ameshtakiwa na Chama cha Soka cha Uingereza (FA) kufuatia mvutano uliotokea kati yake na makocha wa klabu ya Burnley.
Sarri alifukuzwa uwanjani kufuatia kitendo hicho kilichotokea mechi hiyo ya EPL ikielekea kumalizika mapema juma hili uwanjani Stamford Bridge.
Lakini baada ya mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 2-2, kocha huyo alijitetea akidai alirushiwa matusi na wakufunzi wa Burnley.
Sasa ameshtakiwa na amepewa hadi Ijumaa kujitetea kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Taarifa ya FA ilisema: “Maurizio Sarri ameshtakiwa kwa kuvuruga amani wakati wa mechi zilipokuwa zimebakia dakika sita mechi kumalizika.”
Wachezaji Antonio Rudiger wa Chelsea na Billy Mercer waliingilia na kutawanya ugomvi huo kabla ya fujo nyingi kutokea kati ya David Luiz wa Chelsea na Ashley Westwood wa Burnley baada ya mechi kumalizika.
Hata hivyo, Chelsea walitarajiwa kuwasilisha malalamishi yao rasmi kwa FA kabla ya Sarri kujitetea.
Naibu wake, Gianfranco Zola alisema bosi wake walikasirishwa na tabia za makocha wa Burnley ambao walimfokea kwa pamoja.