• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Sterling sasa alilia jezi ya Messi

Sterling sasa alilia jezi ya Messi

Na CHRIS ADUNGO

JAPO anajivunia idadi kubwa ya mataji na zaidi ya mabao 100 katika kipindi ambacho kimemshuhudia akichezea timu ya taifa ya Uingereza mara 56, fowadi Raheem Sterling wa Manchester City hajaridhika.

Kwa mujibu wa mwanasoka huyo wa zamani wa Liverpool, kitakachomridhisha zaidi ni kupata jezi ya nahodha wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi.

Licha ya kumiliki jezi nyingi za wachezaji mbalimbali kabatini mwake, Sterling anahisi kwamba ni jezi ya Messi pekee ndiyo itakayomwamshia ari ya kutamba zaidi kitaaluma.

“Ipo jezi moja zaidi ninayoikamia. Jezi ya Messi. Mara ya mwisho tulipocheza na Barcelona, nilifaulu kupata jezi ya Neymar. Jezi yake ndiyo niliyokuwa nikiitamani zaidi hata kabla ya kushuka dimbani kuvaana nao,” akatanguliza Sterling.

“Nitakapostaafu kwenye ulingo wa soka na kuanza kumakinikia masuala mengine, ni matumaini yangu kwamba nitakuwa nikijivunia idadi kubwa zaidi ya jezi za wanasoka tofauti. Itakuwa fahari kubwa kuteua yoyote kati ya hizo nyingi nizipendazo zaidi niziangike kwenye kuta za nyumba yangu, karibu na kabati langu la makombe,” akaongeza.

Ingawa jezi ya Messi ndiyo anayoitamani sana kwa sasa, ni Ronaldinho Gaucho – nyota wa zamani wa Barcelona – ndiye aliyemchochea zaidi Sterling kuzamia soka alipokuwa mtoto mdogo.

“Nilikuwa shabiki sugu wa Ronaldinho. Alinitia kiu ya kutaka kutamba katika soka. Sidhani kuna video yake yoyote katika Youtube ambayo sijawahi kuitazama kuanzia mwanzo hadi mwisho,” akasema.

“Baada ya kuzitazama video zake, nilikuwa na mazoea ya kuenda uwanjani kuiga niliyojifunza kutoka kwake. Ajabu ni kwamba sikuweza kufaulu licha ya kujaribu tena na tena,” akasisitiza Sterling ambaye kwa sasa anamezewa mate na Real Madrid nchini Uhispania.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Sun, Sterling alifichua kwamba mchezaji anayemhimiza zaidi uwanjani Etihad kwa sasa ni David Silva ambaye anatarajiwa kuagana rasmi na Man-City mwishoni mwa muhula huu na kutua Inter Miami ya Amerika.

“Silva ni mwanasoka mnyenyekevu ambaye siku zote ameazimia kuwashauri chipukizi na kuwaelekeza ipasavyo. Wingi wa mataji anayojivunia ni ithibati tosha kuhusu ukubwa wa kipaji alichokirimiwa,” akasema Sterling kumhusu Silva, 34.

  • Tags

You can share this post!

‘Itakuwa unafiki timu zikimwaga mabilioni tena kusaka...

Covid-19: Sababu za Rais kudinda kulegeza kamba

adminleo