• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Steve Bruce achukua mikoba ya Benitez Newcastle

Steve Bruce achukua mikoba ya Benitez Newcastle

NA CECIL ODONGO

NEWCASTLE United Jumatano ilimteua kocha mahiri Steve Bruce kama mkufunzi wake kwenye mkataba wa miaka mitatu, hii ni kulingana na taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Bruce, raia wa Uingereza atasaidiwa na makocha Steve Agnew na Stephen Clemence ugani St James Park ili kutambisha klabu hiyo iliyokuwa ikinolewa na Mhispania Rafa Benitez misimu mitatu iliyopita.

“Nimefurahi kutunukiwa wadhifa huu adimu tena yenye hadhi kama mkufunzi wa Newcastle United. Hii imekuwa timu yangu tangu utotoni kwa kuwa babangu alikuwa akiishabikia sana. Huu ni wakati spesheli kwangu na familia yangu kutokana na historia ndefu ya kuishabikia Newcastle United,” akasema Bruce.

“Kuna kibarua kigumu sana mbele yetu lakini mimi na benchi yangu ya kiufundi tupo tayari kukabiliana nacho. Tutajitahidi sana kuhakikisha mashabiki wa timu hii wanayafurahia matokeo mazuri,” akaongeza Bruce.

Mkufunzi huyo pamoja na benchi yake ya kiufundi wanatarajiwa kusafiri hadi Uchina ili kukutana na kikosi cha Newcastle ambacho kitakutana na Wolverhampton Wanderers kwenye kipute cha Kombe la Ubingwa wa Bara Asia kinachoendelea nchini humo.

Bruce alianza taaluma yake ya soka akiwajibikia Gillingham FC ambako aliibuka kama kiungo stadi mwenye rekodi na ufundi wa kuyafunga mabao mengi.

Akiwa mchezaji, alishinda Kombe la Ligi(League Cup) na Norwich FC alikocheza kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kujiunga na Manchester na kutwaa ubingwa wa EPL mara tatu, Kombe la FA pia mara tatu, Kombe la Bara Ulaya na pia Kombe la Ligi.

Kati ya mwaka 1996 na 1998 alichezea Birmingham City mara 84 kabla ya kuanza taaluma yake ya ukocha katika Sheffield United FC.

Katika miaka 21 aliyohudumu kama kocha, Bruce amefundisha klabu nane na kuziongoza kushiriki zaidi ya mechi 900 za ligi zao.

You can share this post!

Amuua babake kwa kumkata kichwa, ajitetea alidhani ni mbuzi!

Starlets waamini watakung’uta Malawi kampeni ya Olimpiki

adminleo