Stima yadhihirisha kiu ya kurudi KPL
NA CECIL ODONGO
KLABU ya Western Stima iliimarisha azimio lake la kurejea katika ligi ya KPL baada ya kufungua mwanya wa alama tatu uongozini mwa ligi ya Supa.
Stima walivuna alama tatu muhimu baada ya kuwafunga washiriki wa zamani wa KPL Nakuru All stars mabao 2-1 katika mechi iliyogaragazwa ugani Bukhungu siku ya Jumamosi Agosti 18.
Mabao ya Wanaumeme hao yalitiwa wavuni na mchezaji wa zamani wa Nakuru All Stars Erastus Mwaniki na mwenzake Kevin Okoth huku bao la All Stars likifungwa na Victor Oduor katika dakika ya 90.
Mjini Awendo nambari mbili Nairobi Stima waliwakalifisha Isbania mabao 3-0 yaliyofungwa na mshambulizi wa zamani wa Tusker Stephen Owusu naye Victor Ndinya akafunga mawili.
Nambari tatu Ushuru FC hawakuwa na mechi siku ya Jumamosi na Jumapili nao wapinzani wengine KCB na Bidco wanaoshikilia nafasi ya nne na tano mtawalia wakiagana sare tasa walipochuana katika uwanja wa Camp Toyoyo mnamo Ijumaa Agosti 18.
Nairobi City Stars pia walivuna ushindi mkubwa siku ya Jumamosi kwa kuicharaza StJoseph Youth FC 4-0 na kupanda hadi nafasi ya sita katika msimamo wa jedwali la ligi hiyo.
Baada ya raundi 27 za mechi ya ligi hiyo, GFE 105, Isibania na Green Commandoes zinazoshikilia nafasi tatu za mwisho zinakodolewa macho na shoka la kuteremshwa ngazi hadi ligi ya chini.