• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Suarez awatambisha Uruguay dhidi ya Ecuador kwenye Copa America

Suarez awatambisha Uruguay dhidi ya Ecuador kwenye Copa America

Na MASHIRIKA

SAO PAULO, BRAZIL

WACHEZAJI Luis Suarez na Edinson Cavani walifungia Uruguay mabao muhimu katika ushindi mnono wa 4-0 uliosajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Ecuador katika Kundi C kwenye kinyang’anyiro cha Copa America mnamo Jumapili nchini Brazil.

Nicolas Lodeiro aliwafungulia Uruguay ukurasa wa mabao kunako dakika ya sita kabla ya Ecuador kujipata wakisalia na wachezaji 10 uwanjani baada ya Jose Quintero kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 24.

Uruguay walichuma nafuu kutokana na uchache wa wachezaji wa Ecuador uwanjani na kufunga mabao mengine mawili ya haraka kupitia kwa Cavani na Suarez kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Katika Kundi B, kusuasua kwa Paraguay katika kipindi cha pili kuliwawezesha Qatar ambao watakuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mnamo 2022, kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kusajili sare ta 2-2.

Uruguay ambao wameshinda ubingwa wa Copa America mara nyingi zaidi (15), walianza kampeni zao za makundi kwa matao ya juu mjini Belo Horizonte.

Quintero, 28, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya refa Anderson Daronco kurejelea teknolojia ya VAR kubainisha iwapo alikuwa ameunawa mpira. Awali, nyota huyo alikuwa ameonyeshwa kadi ya manjano kwa kosa la kumkabili visivyo mchezaji Cavani.

Cavani ambaye kwa sasa huvalia jezi za PSG nchini Ufaransa, alicheka na nyavu kunako dakika ya 33 kabla ya Suarez kukizamisha kabisa chombo cha wapinzani wao mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Bao la Suarez lilikuwa lake la 57 akivalia jezi za timu ya taifa ya Uruguay.

Bao la kujifunga

Masaibu ya Ecuador yalizidishwa na beki Arturo Mina wa Yeni Malatyaspor, Uturuki baada ya kujifunga kunako dakika ya 78.

Kulingana na kocha Hernan Dario Gomez wa Ecuador, vijana wake walianza kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara pindi baada ya Quintero kufurushwa uwanjani.

Kwingineko, Paraguay walifunga bao la kwanza dhidi Qatar kupitia penalti ya nyota Oscar Cardozo kabla ya Derlis Gonzalez kupachika wavuni goli la pili.

Hata hivyo, Qatar ambao kwa pamoja na Japan ni waalikwa katika mchuano huo wa timu 12, walirejea mchezoni kupitia kwa Almoez Ali kabla ya Rodrigo Rojas wa Paraguay kujifunga.

Awali, Colombia walikuwa wamepepeta Argentina 2-0 katika mchuano mwingine wa Kundi B.

Leo Jumanne itakuwa ni zamu ya Bolivia kupimana ubabe na Peru katika mchuano mwingine wa Kundi A, huku Chile wakishuka dimbani kuvaana na Japan katika mechi ya Kundi C hapo Jumatano.

You can share this post!

Hofu ya Ebola Kenya

NTSA yashauri washikadau wa matatu

adminleo