Michezo

Talanta Hela ya Kenya yanyakua Kombe la Costa Daurada

March 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TOTO AREGE akiwa BARCELONA, UHISPANIA

TIMU ya wavulana wa umri wa chini ya miaka 19 ya Talanta Hela ya Kenya ndio mabingwa wa toleo la 15 la Kombe la Costa Daurada.

Katika fainali, Kenya ilishinda iliikung’uta Usurbil kutoka Barcelona 3-0 katika Kituo cha Michezo cha Futbol Salou mjini Barcelona, Uhispania.

Mshambuliaji Austin Odongo alifunga mabao mawili kabla ya kiungo Hamisi Otieno kuhakikishia Kenya ushindi kwa bao la tatu katika dakika za lala salama kipindi cha pili.

Odongo na Otieno walitambuliwa kama wafungaji bora wa mashindano, kila mmoja akipokea tuzo ya Kiatu cha Dhahabu.

Chini ya ukufunzi wa kocha Stanley Okumbi, timu hiyo iliheshimiwa kwa kutuzwa medali na Kombe.

Kombe la Costa Daurada. PICHA | TOTO AREGE

Kipa Peter Juma, hakuficha furaha yake katika kuwakilisha Kenya kimataifa na kueleza matumaini ya kuendelea kupigania taifa.

“Nahisi vizuri kuwakilisha Kenya. Maskauti wamekuwa wakitutazama jinsi tulivyocheza na tunatumai kwamba kufikia wakati tunapoondoka Uhispania, tutavutia klabu kubwa za bara Ulaya,” alisema Juma.

Mshambuliaji Elizabeth Mideva alituzwa mfungaji bora wa mashindano akiwa na mabao sita, likiwemo bao la pekee la Kenya katika dakika za ziada za kipindi cha pili dhidi ya Sporting de Portugal ya Ureno. Alituzwa Kiatu cha Dhahabu.

Kipa Christine Adhiambo pia alitambuliwa kama kipa bora wa mashindano. Wasichana pia walitunukiwa medali na kikombe cha timu nambari mbili.