Teknolojia ya mashabiki bandia kutumika EPL
Na CHRIS ADUNGO
LIGI Kuu ya Uingereza (EPL) itakaporejelewa mnamo Juni 17, 2020, watakaofuatilia michuano hiyo runingani watakuwa na chaguo la kusikiliza mbwembwe na kelele za kawaida za mashabiki kila wanaposhangilia au kukemea kila tukio uwanjani.
Huku mechi zikipangiwa kupigwa ndani ya viwanja vitupu kutokana na janga la corona, wasimamizi wa kivumbi cha EPL na wapeperushaji wa michezo hiyo wamepania kutalii ubunifu wa kila aina ili kufurahisha mashabiki wa soka kote duniani.
Teknolojia ya kushirikisha sauti za mashabiki zilizorekodiwa katika mechi za awali tayari inatumika kwa sasa katika soka ya Korea Kusini iliyoanza upya mnamo Mei 2020. Vipaza-sauti vya kisasa huwekwa katika sehemu mbalimbali za uwanja na sauti za ‘mashabiki-hai’ husikika wakiwatilia shime wanasoka.
Teknolojia hiyo iliwahi pia kutumika katika Ligi Kuu ya Ujerumani wakati mabingwa watetezi Bayern Munich walipokwaruzana na Borussia Dortmund kwenye gozi la vidume lililowakutanisha ugani Signal Iduna Park mnamo Mei 26, 2020. Bayern walisajili ushindi wa 1-0 katika mechi hiyo.
INAVYOFANYA KAZI
Sauti za mashabiki zilizonaswa katika matukio ya mechi za zamani zilizokutanisha timu mbili husika zinazochuana kwa mara nyingine zinachanganywa na kelele halisi za wachezaji wakati wa mechi uwanjani.
Prodyusa hutia kwenye kanda kelele za kuashiria hisia za mashabiki kufuatia matukio ya penalti, makabiliano mabaya miongoni mwa wachezaji au mihemko ya kila sampuli wakati refa anaporejelea baadhi ya maamuzi kupitia teknolojia ya video za VAR.
Mashirika ya utangazaji ya Sky Sports, SuperSport na BT Sport yatatumia teknolojia hiyo ya mpya katika mechi zote 92 zilizosalia katika EPL msimu huu kipute hicho kitakaporejelewa mnamo Juni 17, 2020.
Ni matumaini ya vinara wa EPL kwamba hatua hiyo itawapa mashabiki wa kivumbi hicho burudani tosha katika sebule zao nyumbani.