Michezo

Three Lions ya Uingereza yapigiwa upatu kushinda Euro 2024

June 4th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KAMA wewe ni shabiki wa timu ya taifa ya Uingereza, basi huenda ukakula vizuri kwenye Kombe la Ulaya (Euro 2024) kwani Three Lions wanaongoza orodha ya wawaniaji halisi nchini Ujerumani.

Dimba hilo linafanyika Juni 14 hadi Julai 14.

Kwa mujibu wa kompyuta maalum ya Opta, Uingereza inayojivunia wachezaji matata kama Cole Palmer (Chelsea), Ollie Watkins (Aston Villa) na Trent Alexander-Arnold (Liverpool), vijana wa kocha Gareth Southgate wana asilimia 19.9 ya kutawala dimba hilo la mataifa 32.

Waingereza walipoteza dhidi ya Italia katika fainali ya makala yaliyopita.

Mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2022, Ufaransa wanaaminika ndio wanaweza kusimamisha Uingereza.

Wafaransa, ambao pia walifika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018, wana asilimia 19.1 ya kuibuka wafalme wa Euro2024.

Wenyeji Ujerumani pia wako katika orodha ya wagombea halisi wa taji wakiwa na asilimia 12.4 ya kutamba mbele ya mashabiki wao na kufuatiwa na Wahispania (asilimia 9.6) na Wareno (asilimia 9.2).

Waholanzi wana asilimia 5.1 pekee, nao mabingwa watetezi Italia wamepewa asilimia 5.0 ya kuibuka na ushindi. Wabelgiji wana asilimia 4.7 ya kutwaa taji.

Kikosi cha Uingereza:

Makipa – Jordan Pickford (Everton), Aaron Ramsdale (Arsenal), Dean Henderson (Crystal Palace), James Trafford (Burnley);

Mabeki – Kyle Walker, John Stones (Manchester City), Harry Maguire, Luke Shaw (Manchester United), Jarell Quansah, Joe Gomez, Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Kieran Trippier (Newcastle), Jarrad Branthwaite (Everton), Lewis Dunk (Brighton), Ezri Konsa (Aston Villa), Marc Guehi (Crystal Palace);

Viungo – Jude Bellingham (Real Madrid), Declan Rice (Arsenal), Curtis Jones (Liverpool), Jack Grealish, Phil Foden (Manchester City), Kobbie Mainoo (Manchester United), Conor Gallagher (Chelsea), Eberechi Eze, Adam Wharton (Crystal Palace), Anthony Gordon (Newcastle), James Maddison (Tottenham);

Washambulizi – Harry Kane (Bayern Munich), Cole Palmer (Chelsea), Bukayo Saka (Arsenal), Jarrod Bowen (West Ham), Ivan Toney (Brentford), Ollie Watkins (Aston Villa).