• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Timu ya Kamukunji inavyokuza vipaji mitaani

Timu ya Kamukunji inavyokuza vipaji mitaani

Na PATRICK KILAVUKA

Timu ya soka ya Shule ya Upili ya Kamukunji almaarufu kama ‘KAMU’ kutoka kaunti ndogo ya Kamukunji , Kaunti ya Nairobi imeiletea shime katika mashindano ya michezo za shule za sekondari na inashiriki pia katika ligi ya FKF Kauntindogo Tawi la Nairobi Mashariki kama njia ya kukuza vipawa vya kandanda.

Kikosi cha Shule ya Upili ya Kamukunji kaunti ndogo ya Kamukunji,Nairobi kikifanya mazoezi kabla kupiga mechi yake dhidi ya Shule ya upili ya Lang’ata juzi. Picha/Patrick Kilavuka

Imekuwa mwiba kwa timu pinzani katika kaunti ndogo ya Kamukunji hata kutawazwa mabingwa wa soka katika kaunti hiyo na hata kuiwakilishi katika mashindano ya shule za upili na yale ya Copa Coca Cola.

Imewakilishi kaunti ya Kamukunji katika michezo ya shirikisho la Michezo za Shule ya Upili za Kanda ya Nairobi NRSSSA chini ya udhamini wa Copa Coca Cola ingawa ilipoteza kwenye robo fainali kwa ushindi finyu 2-1 dhidi ya watani wao Shule ya Upili ya Langata.

Kocha wa KAMU awapa maagizo wachezaji wake. Picha/ Patrick Kilavuka

Ilianza kutetea ubabe wake katika kaunti ndogo ya Kamukunji bila kupoteza mchuano wowote baada ya kushuka dimbani katika mechi tatu za makundi ambapo iliizaba Eastleigh High 2-0, kuirarura St Johns Pumwani 4-1 kisha kuipokeza Zawadi kichapo cha 4-0 na kufuzu kucheza nusu fainali dhidi ya St Teresa na kuilima 4-1. Hatimaye, ilitua fainali za kaunti ndogo na kuishinda Moi Forces Academy 2-1 hatimaye kupokea mwenge wa kupepetana katika kiwango cha Kaunti ya Nairobi.

Vijana wa KAMU wakifanya mazoezi. Picha/ Patrick Kilavuka

Kuendeleza kampeni yake katika mashindano ya Kaunti, “KAMU” ilipata ushindi wa makundi baada ya kupiga michuano dhidi ya Shule ya Upili ya Shadrack Kimalel na kuibwaga 3-0, Embakasi Garrison kuitandika 4-1 kabla kuagana na Sunflower sare ya 1-1 na kufuzu katika robo fainali kwa kuzoa pointi saba.

Kipa wa KAMU afanyishwa mazoezi ya kupangua mikwaju ya penalti. Picha/ Patrick Kilavuka

Hatimaye, kampeni yake ya kufuzu katika mashindano ya Kanda ilikatizwa baada ya kupoteza katika robo fainali kwa kubamizwa na Langata 2-1.

Chini ya ukufunzi wa mwalimu Lesley Kamwanja na msaidizi wake Hillary Lukasa, wanasoka hawa 20 ambao wanafanyia mazoezi uwanja wa Land Mawe, wanaonesha pia utajiri wa vipawa vyao kwa kushiriki vipute mbalimbali na ligi ya FKF.

Mwaka huu, kikosi hiki kimejitosa katika ligi Kauntindogo, tawi la Nairobi Mashariki na kujipa moyo baada ya kuteremuka uwanjani dhidi ya Homeboys na kuipachika 1-0 uwanjani Mukuru Kwa Reuben kisha kuifunga Jericho Revelation 5-1 uga wa Camp Toyoyo.

Wachezaji wa KAMU washerehekea baada ya kufunga bao. Picha/ Patrick Kilavuka

Kando na kushiriki ligi hiyo, imecheza pia katika kinganganyiro cha Chapa Dimba na kufika nusu fainali ya Kaunti ya Nairobi ingawa ilipoteza dhidi ya Gormahia Youth 3-1.

Timu hii imelea vipaji ambavyo vimesajiliwa na timu mbalimbali baada ya kumezewa mate.

Difenda Gordon Ngeywo yumo zizi la Harambee Stars U-20 na kipa Brian Opiyo yuko Harambee Stars U-17.

Vijana hawa wanafuata maagizo kwenye karatasi kuhusu mbinu za kukabili wapinzani. Picha/ Patrick Kilavuka

Wengine in makipa Stephen Opiyo, Isaac Ouma, Celestine Odera na Bixente Lizarus ambao wamo hema la Gormahia Youth, mlinzi Joseph Odhiambo (MYSA) na kiungo Brian Musa (Nairobi Stima).

Changamoto ya timu hii in ukosefu wa uwanja kudumu wa kufanyia mazoezi hali ambayo inaathiri mpango wake katika kujinoa.

Kwa matokeo bora katika soka, mazoezi ni muhimu kutayarisha misuli kwa mechi. Picha/ Patrick Kilavuka

Mpango? Ni kujishuka kwa mashindano ya mwaka ujao kwani, wangependa kupania kufika fainali za kitaifa za Copa Coca Cola na ya Shule za Upili, kusajili wachezaji na kutwaa Chapa Dimba Kaunti ya Nairobi.

You can share this post!

ERIC MALANDA: Aanzisha timu yenye makali ligini licha ya...

Aladwa aililia korti itamatishe kesi dhidi yake

adminleo