Timu ya Kenya Shujaa wapandishwa ngazi raga za dunia baada ya kucharaza Ujerumani
Na GEOFFREY ANENE
KENYA Shujaa wamewapa Wakenya raha baada ya kurejea kwenye Raga za Dunia kufuatia ushindi mtamu wa 33-15 dhidi ya Ujerumani katika fainali kuu jijini Madrid nchini Uhispania, Jumapili.
Seneta wa Kaunti ya Trans-Nzoia Allan Chesang na mwanaolimpiki na mchezaji muhimu wa zamani wa Shujaa Dennis Ombachi ni baadhi ya mashabiki.
Vijana wa kocha Kevin Wambua wametoka chini mara mbili na kuzamisha Ujerumani kupitia miguso ya nahodha Vincent Onyala, Christant Ojwang, John Okoth, George Ooro na Kevin Wekesa pamoja na mikwaju minne kutoka nahodha Anthony Omondi.
Shujaa walijipata chini 0-5 na 7-10 na pia kusalia watu sita uwanjani dhidi ya saba baada ya Ojwang kulishwa kadi ya njano dakika ya tatu na kukaa nje dakika mbili kabla ya mapumziko.
Lakini, Shujaa hawakufa moyo na wakazima Ujerumani iliyokuwa imewachapa mara mbili katika msimu wa kawaida.
“Ni furaha kubwa tumefuzu kushiriki Raga za Dunia tena. Nashukuru kila mtu aliyeamini katika uwezo wetu,” alisema Onyala.
Shujaa walishiriki Raga za Dunia kutoka msimu 1999-2000 hadi 2022-2023 waliposhushwa ngazi kwa mara ya kwanza kabisa. Wakenya walianza kushiriki duru zote za Raga za Dunia msimu 2004-2005.
Kufika raga ya Challenger 2024, Shujaa walishinda Kombe la Afrika kwa kukanyaga Afrika Kusini 17-12 katika fainali jijini Harare, Zimbabwe mwezi Septemba mwaka jana.
Vijana wa Wambua kisha walitinga fainali kuu ya Challenger baada ya kukamilisha msimu wa kawaida uliojumuisha duru za Dubai, Montevideo na Munich katika nafasi ya pili kwa jumla ya alama 48, nane nyuma ya Uruguay, na kufuatiwa na Chile (46) na Ujerumani (44).
Jijini Madrid, Kenya walichabanga Samoa 19-12 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi B kupitia pointi za Patrick Odongo (miguso miwili) na manahodha Onyala (mguso mmoja) na Omondi (mikwaju miwili) baada ya kujinasua kutoka 12-12 wakati wa mapumziko.
Onyala alipachika mguso wa pekee wakati Shujaa walizamishwa na Uhispania katika mechi ya pili 10-5. Wakenya walimaliza majukumu ya makundi kwa kuangamiza Chile 36-7 kupitia miguso ya Okoth (miwili), Ojwang, Samwel Asati, Onyala na Ooro na mikwaju kutoka kwa Nygel Amaitsa (miwili) na Omondi.
Ujerumani walipoteza 40-19 dhidi ya Amerika, wakapiga Canada 19-14 na kutamatisha Kundi A kwa kulimwa 26-14 na Uruguay.
Baada ya kuwa nje msimu mmoja, Kenya wanarejea katika Raga za Dunia wakiungana na Argentina, Ireland, New Zealand, Australia, Ufaransa, Fiji, Afrika Kusini na Great Britain.
Amerika, Uhispania, Samoa na Canada walijipata katika fainali kuu ya Challenger baada ya kumaliza Raga za Dunia 2023-2024 katika nafasi nne za mwisho.
Amerika walichapa Samoa 40-19 na kujihakikishia msimu mwingine katika Raga za Dunia, nao Uruguay wamerudi juu baada ya msimu mmoja kufuatia ushindi mwembamba wa 12-10 dhidi ya Chile.