Michezo

Timu ya Origi yakabwa ligini

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

HIFK anayochezea Mkenya Arnold Origi Otieno ilitupa uongozi wa mabao mawili ikikabwa na Mariehamn 2-2 mbele ya mashabiki wake kwenye Ligi Kuu ya Finland, Jumamosi.

Origi, ambaye atagonga umri wa miaka 37 hapo Novemba 15, alikuwa michumani mwa HIFK dakika zote 90.

HIFK ilifurahia uongozi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na kiungo Mbrazil Vitinho dakika ya 10 na mshambuliaji John Fagerstrom dakika ya 39.

Wenyeji HIFK walipumzisha wafungaji hao wake dakika ya 69 na kujaza nafasi zao na Matias Hanninen na Nikolas Saira, mtawalia. Uamuzi huo unaonekana ulipunguza makali ya HIFK kutafuta bao na kualika mashambulizi kutoka kwa Mariehamn iliyorejesha goli moja kupitia kwa Gustaf Backaliden dakika ya 77 kabla ya Akseli Pelvas dakika mbili baadaye.

HIFK, ambayo ilikanyaga Mariehamn 3-0 ugenini mwezi Julai, inashikilia nafasi ya tano kwenye ligi hiyo ya timu 12 kwa alama 24 baada ya kusakata mechi 15. Mariehamn inasalia katika mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya saba kwa alama 20.

Katika mechi zingine zilizopigwa kwenye ligi hiyo ya Finland hapo Jumamosi, Ilves na Haka zilitoka 1-1 nayo Inter Turku ikalemewa 1-0 na SJK.