Michezo

Timu ya Rangers kuvurumisha mastaa wapya

January 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

POSTA Rangers itawatangaza wachezaji kadhaa wapya kikosini itakapokabiliana na AFC Leopards hii leo Jumatano mjini Machakos, katika pambano moto la Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Nyota hao wageni ni pamoja na mshambuliaji matata Ezekiel Okare kutoka Ulinzi Stars, ambaye mkataba wake na wanajeshi hao ulimalizika mwezi uliopita.

Okare alijiunga na Ulinzi mnamo 2018 akitokea Sofapaka FC.

Mtandao rasmi wa klabu ya Ulinzi ulisema: “Ezekiel Okare ameondoka na kujiunga na Posta Rangers baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika. Tunamtakia kila la heri popote aendako.”

Mbali na Okare, Posta Rangers pia imefanikiwa kuzipata huduma za Humphrey Okoti na Collins Okumu kutoka Sony Sugar FC, pamoja na Clinton Kisiavuki aliyeagana na timu ya Kenya Commercial Bank (KCB) majuzi.

Okare, Okumu na Kisiavuki wamesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu kila mmoja.

Hata hivyo, muda wa mkataba wa Humphrey Okoti haukutangazwa rasmi.

Mbali na kutwaa mastaa hao matata, Rangers pia iliandikisha upya mikataba ya wachezaji wake Charles Odette na Simon Mbugua.

Mikataba hiyo mipya itakuwa ya miaka mitatu kwa kila mchezaji.

Okumu na Okoti hawajacheza kwa miezi mitatu tangu klabu ya Sony Sugar iondolewe ligi kuu ya KPL, kwa kukosa kufika uwanjani mara tatu mfululio.

Kwingineko, Mathare United imeagana na mshambuliaji Chris Ochieng baada ya mkataba wake kufikia kikomo.

Mwanasoka huyo alithibitisha jana kwamba ameondoka, baada ya kuichezea timu hiyo ya ligi kuu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kupitia kwa mtandao wake wa kibinafsi, Ochieng alisema: “Ningependa kuwashukuru mashabiki na wachezaji wa Mathare kwa kuniunga mkono wakati wote nilipokuwa klabuni. Nawapenda nyote. Nawatakieni kila la heri.”

Ochieng alijiunga na Mathare mnamo 2017 akitokea Park Road FC. Kuondoka kwake ni pigo kuu hasa baada ya kusaidia klabu hiyo kufunga mabao 18 msimu huu.

Ochienge, hata hivyo, hakueleza hatua itakayofuata baada ya kuondoka Mathare.

Hii itakuwa mechi ya 16 kwa Leopards ambao majuzi waliibuka na ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Zoo Kericho mjini Kakamega.

Vijana hao wa kocha Anthony Kimani wanashikilia nafasi ya saba katika jedwali wakiwa na pointi 25.

Mabingwa watetezi Gor Mahia wanaongoza msimamo wa ligi wakifuatiwa na Tusker FC, kwa pointi 32 na 31 mtawaliwa.