Michezo

Timu za Kenya na TZ kuwania ubingwa wa SportPesa Super Cup

May 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MAKALA ya pili ya soka ya SportPesa Super Cup yataleta pamoja Gor Mahia, AFC Leopards, Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz (Kenya) na Yanga, Singida United, Simba SC na Jeshi la Kujenga Uchumi (Tanzania).

Mshindi wa makala haya atasafiri nchini Uingereza kumenyana na Everton katika uwanja wao wa nyumbani, Goodison Park.

Wadhamini, kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa walitangaza Alhamisi kwamba mashindano haya yatandaliwa Juni 3-10 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

Sharks na Homeboyz zimejumuishwa katika mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa. Zinachukua nafasi za Tusker na Nakuru AllStars. Jeshi la Kujenga Uchumi imejaza nafasi ya Jang’ombe.

Gor, Leopards, Yanga, Simba na Singida zilishiriki makala ya kwanza yaliyoandaliwa jijini Dar es Salaam. Mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor, walipepeta mahasimu wao wa jadi Leopards 3-0 katika fainali na kujikatia tiketi ya kukabiliana na Everton kutoka Uingereza.

Gor ilizamishwa 2-1 na Everton jijini Dar es Salaam. Kieran Dowell na Wayne Rooney walifungia Everton naye Jacques Tuyisenge akapachika bao la kufutia machozi la Gor.

Gor, ambayo ililemewa na Hull City kwa njia ya penalti 4-3 uwanjani Kasarani katika mchuano mwingine wa kimataifa wiki mbili zilizopita, inapigiwa upatu kutwaa taji la Super Cup. Hull pia inadhaminiwa na SportPesa na ziara yake hiyo ilifanikishwa na kampuni hiyo.

Mgao wa tuzo:

Robo-fainali Sh250,000

Nambari nne Sh500,000

Nambari tatu Sh750,000

Nambari mbili Sh1,000,000

Mabingwa Sh3,000,000 & tiketi ya kuvaana na Everton uwanjani Goodison Park