Michezo

Timu za Voliboli ya Ufukweni kushiriki Kombe la Afrika nchini Morocco

June 16th, 2024 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU za taifa za voliboli ya Ufukweni, wanaume na wanawake zimeratibiwa kuondoka leo jioni kuelekea nchini Morocco kushiriki mechi za Kombe la Afrika (CAVB).

Ngarambe hiyo pia itatumika kupigania tikiti ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki 2024 Paris, Ufaransa. Shindano hilo litakaloandaliwa jijini Tetouan limepangwa kuanza Juni 19 hadi 23.

”Tumekuwa kwenye ufuo wa Flamingo Pride Inn jijini Mombasa tulikoshiriki mazoezi ya wiki moja ambapo wachezaji wetu wapo tayari kwa kibarua kilicho mbele yao,” alisema kocha wa timu ya wanaume, Ibrahim Oduor.

Aliongeza kuwa watahitaji kupambana kwa udi na uvumba kwenye michuano hiyo huku wakilenga angalau timu moja ifuzu kwa Olimpiki. Anaamini wamekaa vizuri kwa kipute hicho ingawa walianza mazoezi yao kuchelewa.

Baada ya mazoezi hayo kocha huyo na mwenzake wa kikosi cha wanawake, Salome Wanjala walichuja wachezaji wawili na kusalia na wawili. Timu ya wanaume itajumuisha; Edward Kibet wa Jeshi la Ulinzi (KDF) na Brian Melly wa Kenya General Service (GSU).

Waliotemwa wakiwa ni Alphas Makuto na Jairus Kipkosgei, wote ni wa Kenya Prisons. Wanawake watakuwa; Gaudencia Makokha na Naomi Too wote wa Kenya Pipeline. Waliotemwa ni Sharleen Sembei (KCB) na Yvonne Wavinya wa Kenya Prisons.

Itakumbukwa kuwa Gaudencia aliwahi kushiriki Olimpiki za mwaka 2020 zilizoandaliwa Tokyo, Japan. Alidokeza kwamba kwenye michuano hiyo wanatarajia ushindani mkali kutoka kwa wenyeji Morocco, Misri, Tunisia, Botswana, Afrika Kusini na Msumbuji.

Pia Rwanda, Mauritius,Ghana na Namibia ni kati ya nchi zingine zinazo tarajiwa kushiriki kipute hicho.