Michezo

Top 8 sasa kuwa Super 16

July 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limefichua mpango wa kurejesha kipute cha Top Eight kuanzia msimu ujao wa 2020-21.

Mashindano hayo ambayo yalikuwa yakikutanisha klabu zinazokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ndani ya mduara wa nane-bora kila msimu yalianzishwa mnamo 2011. Hata hivyo, yalisitishwa katika mwaka wa 2016 kutokana na uchechefu wa fedha baada ya wadhamini SuperSport ya Afrika Kusini kujiondoa. Hatua hiyo ya SuperSport ilichangiwa na maamuzi ya FKF kupanua ligi ya KPL kutoka vikosi 16 hadi 18.

Hata hivyo, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF, amesisitiza kuwa kivumbi hicho kitarejea kuanzia msimu ujao wa 2020-21 na kitaitwa sasa Super 16 huku Ligi Kuu ikiitwa BKPL Super baada ya shirikisho kupata ufadhili wa Sh1.2 bilioni kutoka kampuni ya kampuni ya kamari ya Bet King nchini Nigeria. Udhamini huo utadumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na kila kikosi cha Ligi Kuu ya BKPL Super kitakuwa kikipokezwa Sh8 milioni kwa msimu.

“Kipute cha Super 16 kitachukuwa nafasi ya kile kilichojulikana kama Top Eight kuanzia msimu ujao wa 2020-21. Itamaanisha kwamba vikosi vinane vya kwanza katika Ligi Kuu vitashindana na vikosi vinane vya Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL),” akasema Mwendwa anayetazamia kuhifadhi uenyekiti wa FKF katika uchaguzi mkuu ujao wa shirikisho hilo.

Zaidi ya kudhamini soka ya Super 16 na BKPL Super, kampuni ya Bet King pia itakuwa ikimtuza Mchezaji Bora na Kocha Bora wa mwezi katika Ligi Kuu ya humu nchini na pia kufadhili tuzo za mwisho wa kila msimu kwa wanasoka, makocha na vikosi vilivyotia for a zaidi.

FKF na Bet King watashirikiana pakubwa na Chama cha Wanahabari wa Spoti nchini (SJAK) ambacho kimekuwa kikiendesha programu huru ya kuteua wachezaji na makocha bora wa kutuzwa kila mwezi chini ya udhamini wa kampuni ya bima ya Fidelity na kampuni ya vyombo vya elektroniki ya LG.

Mwendwa pia amewakashifu vikali wapinzani wake baada ya wawaniaji wanne wa urais wa FKF kuonya mashirika mbalimbali dhidi ya kurasimisha dili zozote za kibiashara na FKF hasa kipindi hiki ambapo uchaguzi mpya unakaribia.

Mnamo Alhamisi, Lodvick Aduda, Nicholas Musonye, Sammy Sholei na Twaha Mbarak waliitaka Tume ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Idara ya Upelelezi wa Kesi za Jinai (DCI) kumsukuma Mwendwa zaidi aelezee jinsi alivyotumia Sh244 milioni zilizotolewa na serikali kwa minajili ya timu ya taifa ya Harambee Stars kushiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri.

“Sina muda na watu ambao wamekuwa wakipanga kuanguka kwangu katika kumbi za hoteli mbalimbali na mahakama. Tunasubiri mwelekeo wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuhusu uchaguzi ujao kisha nikutane nao debeni,” akasema Mwendwa.