Michezo

Tottenham kuvaana na Shkendija Europa League

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho wa Tottenham Hotspur amesema ameanza sasa kuamini ukubwa wa uwezo wa sajili mpya Tanguy Ndombele baada ya Mfaransa huyo kufunga bao la dakika ya mwisho lililowasaidia waajiri wake kubandua Lokomotiv Plovdiv ya Bulgaria kwenye Europa League.

Tottenham waliponea chupuchupu kudenguliwa mapema kwenye kipute hicho kilichoshuhudia Lokomotiv ya Bulgaria wakisalia kutegemea wanasoka tisa pekee baada ya Lima Almeida na Birsent Karagaren kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika za 78 na 79 mtawalia.

Georgi Minchev aliwaweka Lokomotiv Plovdiv kifua mbele kunako dakika ya 72 kabla ya Harry Kane kusawazisha mambo katika dakika ya 80 na Ndombele kufunga bao la ushindi dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Ndombele, 22, alisajiliwa na Tottenham kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa kwa kima cha Sh7.5 bilioni mnamo Agosti 2019. Tangu wakati huo, sogora huyo alikuwa amewajibishwa katika mechi 17 pekee kwenye mashindano yote ya msimu wa 2019-20 kutokana na wepesi wa kupata majeraha na kushtumiwa na kocha Mourinho.

“Tanguy anaanza kuimarika. Nimeanza sasa kuamini uwezo wake,” akasema Mourinho ambaye mnamo Machi 2020, alitaka kiungo huyo “kujituma zaidi” mechini.

“Ushawishi wake uwanjani haukuhisika kabisa msimu jana. Lakini kwa sasa amejitambua na anajitahidi sana hata mazoezini. Amepona jeraha na bao alilofunga litampa msukumo zaidi wa kusajili matokeo ya kuridhisha,” akasema.

Kutokana na ushindi wa Tottenham, Mourinho kwa sasa anajiandaa kuongoza masogora wake kuvaana na Shkendija ya Macedonia mnamo Alhamisi ya Septemba 24 katika mechi ya raundi ya tatu ya mchujo wa Europa League.

Kabla ya hapo, Tottenham watapepetana na Southampton kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 20 kisha kuchuana na Leyton Orient katika gozi la EFL Cup mnamo Septemba 22, 2020.

Iwapo wataibuka washindi wa mechi mbili za EFL na Europa League, basi Tottenham watasakata tena michuano mitatu chini ya siku saba wiki inayofuatia baada ya Septemba 27, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO