• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Tottenham wafunga mawili na kuendeleza ubabe wao dhidi ya Arsenal katika EPL

Tottenham wafunga mawili na kuendeleza ubabe wao dhidi ya Arsenal katika EPL

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuwapokeza Arsenal kichapo cha 2-0 mnamo Disemba 6, 2020.

Ni mchuano ulioshuhudia mshambuliaji na nahodha wa Tottenham, Harry Kane akiweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa gozi la London Kaskazini kati ya Arsenal na Tottenham ambao ni watani wakuu kwenye soka ya Uingereza.

Kane ambaye ni raia wa Uingereza sasa anajivunia mabao 11 kutokana na mechi za EPL kati ya Tottenham na Arsenal na goli lake lilikuwa la 250 kitaaluma tangu aanze kutandaza soka katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Fowadi Son Heung-min aliwaweka Tottenham kifua mbele katika dakika ya 13 kabla ya Kane kufungia waajiri wake bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Ushirikiano mkubwa kati ya wawili hao ulitatiza kipa Bern Leno wa Arsenal na ukawapa mashabiki wa Tottenham waliokuwa wakirejea uwanjani baada ya siku 277 kila sababu ya kuonea kikosi chao fahari.

Licha ya Arsenal kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha kwanza, ni Tottenham ndio waliotumia vizuri fursa chache walizozipata na kuwaadhibu wageni wao kirahisi.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal walimpoteza kiungo Thomas Partey kupitia jeraha mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ushindi wa Tottenham ambao pia waliwapiga Manchester City 2-0 mnamo Novemba 21, ni ufanisi ambao kwa sasa unawafanya kuwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu chini ya mkufunzi Jose Mourinho. Iwapo Tottenham watatwaa ubingwa wa EPL, basi itakuwa mara yao ya kwanza kufanya hivyo baada ya miaka 60.

Kwa mara nyingine, Mourinho hakumwajibisha fowadi Gareth Bale licha ya mashabiki waliofika uwanjani na kumuona kwa mara ya kwanza tangu aagane na Real Madrid kwa mkopo, kumshangilia akipiga njaramba nje ya uwanja. Badala yake, Tottenham walisalia kutegemea pakubwa maarifa ya Son na Kane kwenye safu ya mbele.

Mbali na Son na Kane, mchezaji mwingine aliyeridhisha zaidi kambini mwa Tottenham ni sajili mpya Pierre-Emile Hjobjerg aliyesalia imara katika safu ya ulinzi na kuwadhibiti vilivyo wavamizi wa Arsenal.

Matokeo ya Arsenal yaliwatupa hadi nafasi ya 15 kwa alama 13 kutokana na mechi 11 zilizopita za EPL. Ni pengo la pointi 11 ambalo kwa sasa linawatenganisha Tottenham na Arsenal ambao wamepoteza mechi sita kati ya tisa zilizopita ligini.

Tottenham wanajivunia sasa kushinda debi za London Kaskazini mara tatu mfululizo baada ya Disemba 1992 na Mei 1993 kisha Aprili 2010 na Novemba 2010.

Arteta anakuwa kocha wa pili wa Arsenal baada ya Bertie Mee mnamo 1966-67 kupoteza debi mbili za kwanza za London Kaskazini.

  • Tags

You can share this post!

Seneti kuamua jinsi Sonko atakavyojitetea

Wakazi wa jiji wajiandaa kufurika vijijini kwa Krismasi