Michezo

Tuchel akataa dili ya kunoa Man U, Pep naye akikonyezewa jicho na Barca

June 11th, 2024 1 min read

KOCHA Thomas Tuchel amejiondoa kwenye orodha ya makocha ambao wanatafutwa kuchukua majukumu ya Manchester United msimu ujao.

Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich na Chelsea alikuwa miongoni mwa wakufunzi waliopigwa daruni na Red Devils ili kumrithi Erik ten Hag iwapo atatimuliwa baada ya kuwa usukani kwa misimu miwili sasa.

Tathmini ya baada ya msimu bado haijafikia tamati yake Ten Hag, wala hajajua ikiwa bado atakuwa mkufunzi ugani Old Trafford msimu ujao.

Inafahamika kuwa Tuchel alikutana na bwanyenye wa United Sir Jim Ratcliffe nchini Ufaransa.

Hata hivyo, Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 50 anataka kupunga hewa baada ya kuondoka Bayern mwisho wa msimu uliokamilika mwezi jana.

Tuchel amewahi pia kunoa klabu za Borussia Dortmund ya Ujerumani na Paris St-Germain ya Ufaransa.

Man United wamehusishwa na makocha kadhaa akiwemo wa zamani wa Chelsea na Tottenham, Mauricio Pochettino, Thomas Frank wa Brentford, Graham Potter na pia mkufunzi wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate.

Southgate ana mkataba kambini mwa timu ya taifa hadi mwisho wa mwaka.

Naye mkufunzi wa Manchester City, Pep Guardiola, ametupilia mbali uwezekano wowote wa kurejea kuinoa Barcelona.

Mkataba wake Man City utakamilika Juni 2025 na huenda msimu ujao ukawa mwisho wake ugani Etihad.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kurejea Barcelona, Guardiola alisema: “Mlango huo umefungwa kabisa!”

Barca walimaliza msimu wa 2023–24 bila kushinda taji lolote.

Walimfuta mchezaji wao wa zamani Xavi Hernandez baada ya kumuomba asiondoke alipotangaza Januari kwamba angeng’atuka mamlakani.

Vigogo hao wa Uhispania sasa wamemteua kocha wa zamani wa Bayern na timu ya taifa ya Ujerumani, Hansi Flick.