• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Tulichambua Zambia vizuri sana na tuna matumaini ya kufuzu – kocha wa Tanzania

Tulichambua Zambia vizuri sana na tuna matumaini ya kufuzu – kocha wa Tanzania

NA LABAAN SHABAAN

ULIMBUKENI wa Taifa Stars wa Tanzania haukuwasaidia kuwanyuka Chipolopolo wa Zambia lakini motisha yao iliwashindia pointi muhimu.

Taifa Stars walitoana kijasho na Chipolopolo wakiwa na rekodi duni ya sare moja na kubwagwa mara sita katika makala matatu yaliyopita.

Walisakata mechi hii chini ya Mkufunzi Msaidizi Hemed Suleiman Morocco baada ya Kocha Adel Amrouche kupigwa kalamu na Shirikisho la Kandanda la Tanzania (TFF).

Ni baada ya shirikisho la Kandanda la Afrika (CAF) kumpiga marufuku ya mechi nane Amrouche kwa kudai timu ya Morocco inakula njama na CAF kupanga mechi.

Hemedi alisema vijana wake walipoteza umakinifu dhidi ya timu ambayo ilikuwa na uwezo wa kuwasambaratisha wakati wowote.

“Ninajua timu hii. Tuliwafuata na kuwachambua vizuri sana. Katika soka, timu zenye wachezaji 10 huwa hatari sana nasi tukakosa kuwa makini na tukafungwa dakika ya mwisho,” aliungama Hemedi.

Kabla ya mchuano huu, Tanzania walionyesha mchezo wa kuridhisha dhidi ya nyota wa Kombe la Dunia waliofika nusu fainali, Morocco, licha ya kuzabwa mabao matatu kwa nunge.

Tanzania iliambulia sare ya bao moja waliposhuka dimbani kukabana koo na Zambia Jumapili usiku katika Kipute cha Kinyang’anyiro cha Kandanda Afrika makala ya 2023 (AFCON).

Simon Msuva aliweka Tanzania kifua mbele dakika ya 11 wakiishi na matumaini ya kuibuka washindi hadi dakika ya 88.

Hapo ndipo Patson Daka aliruka na kupiga mpira wa kichwa hadi kimiani alipokutana na mkiki wa kona.

Chipolopolo walienda mapumzikoni bila mchezaji mmoja baada ya Roderick Kabwe kurambishwa kadi nyekundu alipocheza visivyo.

Hali hii ilimkirihisha Kocha wa Zambia Avram Grant aliyesononeka kwa matokeo ya mechi hii.

“Matokeo haya ni ya kuvunja moyo. Tulijua hautakuwa mchuano rahisi baada ya kuona Tanzania walipocheza dhidi ya Morocco. Tulianza vizuri lakini baada ya kufungwa bao la mapema, mbinu yetu ikabadilika hasaa tulipopewa kadi nyekundu,” alisema.

Naye staa wa Chipolopolo, Daka, alisifu wachezaji wenzake kwa kuwa thabiti wakiwa kasoro mchezaji mmoja.

“Tulifaa kupata pointi hii na ninapenda kutoa heko kwa kikosi hiki,” akadokeza Daka akifichua wamekuwa wakifanya mazoezi bila mchezaji mmoja kwa kusudi ili wajiandae kwa matukio sampuli hii.

Zambia wana alama mbili katika kundi F baada ya kucheza mechi mbili.

Ili kuweka hai matumaini ya kushiriki mkondo wa 16, Chipolopolo wanahitaji angalau sare dhidi ya Morocco, japo itategemea matokeo ya mechi kati ya Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Katika Kundi F, Morocco wanaongoza kwa alama 4, Zambia na DRC wana alama mbili mbili na Tanzania wakiwa wa mwisho kwa alama moja.

Timu zote zina matumiani ya kuingia raundi ya mwondoano watakaposhiriki mechi ya mwisho ya makundi Jumatano Januari 24, 2024 nchini Ivory Coast.

  • Tags

You can share this post!

DeSantis ajiondoa na kuunga Trump kwa urais Amerika

DONDOO: Mdogo kazini afutwa kazi akibishania mwanamke na...

T L