Michezo

Tuma maombi ya kazi upya, kocha wa Harlequins aambiwa

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA mkuu wa Kenya Harlequins, Dominique Habimana, atalazimika sasa kutuma upya maombi ya kazi ili kuhifadhi wadhifa wake kambini mwa kikosi hicho cha raga ambacho kimetangaza nafasi hiyo kuwa wazi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti Michael Wanjala, Harlequins walimwachilia Habimana mwezi mmoja uliopita na yuko huru kuomba upya nafasi ya kazi ya ukufunzi kikosini mwao iwapo angali na azma ya kuendelea kutoa huduma zake.

Habimana ambaye anajivunia kuhudumu kambini mwa Kenya Simbas kwa kipindi kirefu akiwa kocha, amewahi pia kuwaongoza Nakuru RFC kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Raga ya Kenya Cup mnamo 2013 na 2014 mtawalia.

Ingawa hivyo, mbinu zake za ukufunzi hazijafaulu msimu huu baada ya kushuhudia Harlequins wakiambulia nafasi ya tisa kwenye jedwali la Kenya Cup na hivyo kukosa kufuzu kwa mchujo.

Kwa mtazamo wake, matokeo duni ya kikosi chake ni maandalizi mabaya ya Harlequins kabla ya mwanzo wa msimu huu.

“Mbali na panda-shuke tele za kifedha zilizotunyima nafasi ya kufanya mambo mengi ya muhimu muhula huu, kikosi pia hakikushiriki maandalizi bora kwa minajili ya msimu wa 2019-20,” akasema.

Wanjala ameshikilia kwamba usimamizi wa Harlequins kwa sasa unapania kuimarisha zaidi benchi ya kiufundi hasa baada ya kutangaza pia nafasi za kazi kwa kocha wa akademia na mkufunzi wa mazoezi ya viungo vya mwili.

Kamati Kuu ya Kiufundi ya Harlequins ndiyo itakuwa na usemi wa mwisho kuhusu watakaojitwalia nafasi hizo zilizotangazwa. Walio na azma ya kuhojiwa kwa minajili ya kuzingatiwa katika mojawapo ya nafasi hizo wana hadi leo Jumanne kutuma maombi yao. Wakaoteuliwa baada ya mahojiano watafichuliwa Juni 20, 2020.

Harlequins ambao wanajivunia kutoa wanaraga matata ambao wamekuwa wakiviwajibikia vikosi vya kitaifa vya Shujaa, Simbas na Chipu, tayari wameanza mpango wa kujifua kwa minajili ya msimu ujao.

Kufikia sasa, wamefaulu kuwasajili wanaraga Mark Wandetto kutoka Homeboyz na Leroy Mbugua wa Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

“Tuna kundi la wachezaji chipukizi wanaojivunia utajiri wa talanta na vipaji. Tunalenga kuunga kikosi kilicho na mseto wa wanaraga chipukizi na wazoefu kadri tunavyopania kuingia ndani ya mduara wa sita-bora jedwalini msimu ujao,” akaongeza Wanjala kwa kufichua kwamba wamepata mdhamini mpya atakayefichuliwa na kikosi mwezi ujao.

Baadhi ya chipukizi ambao Harlquins wanalenga kuwakweza kutoka akademia hadi kikosi cha kwanza kwa minajili ya msimu ujao ni nahodha wa kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 20 Boniface Ochieng, Elisha Koronya na Melvin Thairu waliokuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Simbas mnamo 2019.

Katika kivumbi cha msimu huu, Harlequins walisajili ushindi katika mechi tano na kupoteza jumla ya michuano 11 katika matokeo yaliyowashuhudia wakijizolea alama 28 pekee.