Tumaini, Isiolo Starlets mibabe wa Chapa Dimba Mashariki
Na JOHN KIMWERE
TUMAINI School FC na Isiolo Starlets zimetangazwa mafahali na malkia wa Chapa Dimba na Safaricon Season Three, katika Mkoa wa Mashariki baada ya kunyamazisha wapinzani wao katika fainali zilizopigiwa Kenyatta Stadium, Machakos.
Tumaini ya Makueni iliikomoa Black Panthers ya Meru mabao 4-1 katika fainali ya kusisimua. Nayo Isiolo Starlets iliibuka wakali mbele ya Chuka University ilipoilaza mabao 3-2.
Fainali ya wavulana ilianza kwa kasi ambapo Tumaini ilijipatia bao la kwanza kunako dakika ya nne lililojazwa kimiani na Yasin Mohamed, kabla ya kuongeza mabao mawili dakika ya 19 na 47 na kutinga ‘hat trick.’
Hata hivyo wachezaji wa Black Panthers walionyesha kwamba wao sio mende ambapo walijitahidi kwa udi na uvumba na kufunga bao la kufuta machozi lililopachikwa kimiani na Enow Abdumalik dakika ya 83.
Dakika tano baadaye Tumaini iliongezea bao la nne na la kufunga shughuli lililojazwa kimiani na Kapirante Moris.
Kwa wasichana, Susan Wanjeri alionyesha ustadi wake dimbani ambapo aliifungia Chuka University bao la kwanza kunako dakika ya tatu.
Hata hivyo wachezaji wa pande zote waliendelea kuonyesha ujuzi wao na dakika 30 baadaye Rebeca Nkirote alitikisa wavu mara moja na kusawazishia Isiolo Starlets.
Kipindi cha pili vigoli wa Isiolo Starlets walirejea dimbani kwa kusudi moja kuhangaisha wenzao na kuhakikisha wametwaa ubingwa huo na kusonga mbele.
Hilda Wanjiku na Nasibo Ibrahim kila mmoja alifungia Isiolo Starlets bao moja dakika ya 53 na 57.
Hata hivyo Susan Wanjeri aliendelea kuonyesha ubabe wake ambapo aliongozea Chuka University bao la pili lakini walishindwa kuwapiku wapinzani wao.
”Nashukuru wachezaji wangu kwa kusonga mbele sasa tunaanza maandalizi ya kushiriki fainali za kitaifa,” alisema kocha wa Isiolo Starlets, Hussein Wako.
Kocha huyo aliongeza kuwa walikuwa wamejipanga vizuri kukabili wapinzani wao kiume hawa wakilenga kubeba taji hilo pia kutwaa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa.
Kadhalika koccha huyo alisema kuwa nao wanataka kupigana mwanzo mwisho kuwinda ushindi wa kitaifa hili kutuzwa kitita cha Sh1 milioni.
NUSU FAINALI
Kwenye nusu fainali, wavulana wa Tumaini School waliadhibu Biashara FC kutoka Moyale kwa mabao 7-1, nayo Black Panthers ilibamiza St Daniels ya Chuka kwa magoli 7-6 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 3-3 katika muda wa kawaida.
Wasichana wa Chuka University walikomoa Ngakaa Talents mabao 2-1 nayo Isiolo Starlets ilidhalilisha Mabuu Queens kutoka Moyale kwa mabao 8-0.
TIKETI ZA FAINALI ZA KITAIFA
Tumaini FC na Isiolo Starlets kila moja ilituzwa Sh200,000, nazo Black Panthers na Chuka University kila moja ilipokea Sh100,000. Kando na hayo, mabingwa hao walibeba tiketi za kushiriki fainali za kitaifa zitakaoandaliwa mjini Mombasa mwezi Juni mwaka huu.
WACHEZAJI BORA
Nao Yasin Mohamed (Tumaini School) na Susan Wanjeri (Chuka University) kila mmoja aliibuka mchezaji anayeimarika kitengo cha wavulana na wasichana mtawalia.
Kwa mara nyingine wawili hao waliibuka wafungaji bora baada ya kutupia kambani mabao 7 na 4 mtawalia.
Kwa mlinda lango bora, tuzo hiyo iliendea Samuel Milton (Tumaini) na Riziki Fatuma (Isiolo Starlets) kitengo cha wavulana na wasichana mtawalia.
Mabingwa hao, Tumaini School na Isiolo Starlets wamejiunga na wenzao kutoka maeneo mengine ambazo zimefuzu kushiriki fainali za kitaifa.
Wavulana wamejiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.
Wasichana wamejiunga na Falling Waters kutoka Mkoa wa Kati na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.