Michezo

Tumaini, Isiolo Starlets zavuna Chapa Dimba

February 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

WAVULANA wa Tumaini FC na wasichana wa Isiolo Starlets walivuna ushindi mnono kwenye nusu fainali za Mkoa wa Mashariki kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three, zilizopigiwa uwanja wa Kenyatta Stadium, mjini Machakos.

Timu ya Shule ya Tumaini kutoka Makueni iliadhibu Biashara FC kutoka Moyale kwa mabao 7-1. Nayo Mabuu Queens kutoka Moyale ilinyoroshwa kwa mabao 8-0 na Isiolo Starlets ya Isiolo.

Kwenye nusu fainali ya pili kwa wavulana, Black Panthers ya Meru ilijikatia tikiti ya fainali iliponyamazisha St Daniels ya Chuka kwa magoli 7-6 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 3-3 katika muda wa kawaida.

Nao wasichana wa Chuka University walikomoa Ngakaa Talents mabao 2-1 na kujipatia tikiti ya fainali. Ngakaa Talents ilikosa nafasi ya kusonga mbele licha ya kwamba ndio iliyokuwa bingwa wa taji hilo kwenye mashindano ya makala ya Chapa Dimba na Safaricom Season One.

Hassan Kalla wa Biashara FC(kulia) akijaribu kumpiga chenga mpinzani wake, Matipe Melton wa Tumaini FC kwenye nusu ya wavulana katika Mkoa wa Mashariki kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom, Season Three uwanjani Kenyatta Stadium, mjini Machakos. Tumaini ilishinda mabao 7-1. Picha/ John Kimwere

Wavulana wa Tumaini walionyesha mechi safi na kufanikiwa kubebesha wapinzani wao kapu la mabao na kujihakikishia tikiti ya kushiriki fainali.

Yasin Mohamed na Kapirante Moris wa Tumaini walitikisa wavu mara nne na mara mbili mtawalia huku Moses Kinama akifunga bao moja. Nayo Biashara FC ilipata bao la kufuta machozi kupitia juhudi zake Abdirahman Mustapha.

Katika muda wa kawaida baina ya Black Panthers na St Daniel walifungaji wa Black Panthers walikuwa Preston Mwenda mabao mawili naye Denis Muriithi aliitingia goli moja. Jared Owili wa St Daniels alicheka na wavu mara mbili naye Milton Lesuda aliangusha kimiani kombora moja safi.

Nao warembo wa Isiolo Starlets walishusha mechi safi na kuwazidi maarifa wapinzani wao . Nasibo Ibrahim, Nasibo Wario na Halima Tadicha kila mmoja alifunga mara mbili huku Kula Dida na Guyatu Halaike kila mmoja akijaza kimiani bao moja.

Getrude Ondimu wa Chuka University (kulia) akishindana na Pauline Akoth wa Ngakaa Talent kwenye nusu ya wasichana katika Mkoa wa Mashariki kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom, Season Three uwanjani Kenyatta Stadium, mjini Machakos. Chuka ilishinda mabao 2-1. Picha/ John Kimwere

”Nashukuru kwa ushindi huo uliochangiwa pakubwa na bidii ya wachezaji wangu maana waliteremka dimbani kwa kusudio moja kutesa na kubeba tikiti ya kushiriki fainali,” alisema kocha wa Isiolo Starlets, Hussein Wako.

Kikosi cha Chuka University kilipata mafanikio hayo kupitia juhudi zake Susan Wanjeri aliyetikisa wavu mara mbili naye Samantha Adhiambo alifungia Ngakaa Talents bao la kufuta machozi.

Kando na kutangazwa mabingwa wa eneo hilo washindi katika fainali watatuzwa kitita cha Sh200,000 na wafadhili wa kipute hicho kampuni ya Safaricom. Kadhalika watatwaa tikiti za kushiriki fainali za kitaifa ambazo zimeratibiwa kuandaliwa mjini Mombasa mwezi Juni mwaka huu.

Hassan Kalla wa Biashara FC(kulia) akijaribu kumpiga chenga mpinzani wake, Matipe Melton wa Tumaini FC kwenye nusu ya wavulana katika Mkoa wa Mashariki kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom, Season Three uwanjani Kenyatta Stadium, mjini Machakos. Tumaini ilishinda mabao 7-1. Picha/ John Kimwere

Washindi wa eneo hilo watajiunga na wenzao kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa. Wavulana watajiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.

Wasichana watajiunga na Falling Waters Mkoa wa Kati na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.