TUMAINI LA KENYA: Fainali za mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake
Na CHRIS ADUNGO
NYOTA Hellen Obiri, Lilian Kasait na Margaret Chelimo wanabeba leo Jumamosi matumaini ya Kenya ya kujinyakulia medali katika fainali za mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake kwenye Riadha za Dunia zinazoendelea jijini Doha, Qatar.
Obiri ambaye ni malkia wa Afrika, Jumuiya ya Madola na Dunia katika mbio hizo, ni mmoja wa watimkaji ambao walitegemewa sana kuzolea Kenya nishani katika mbio za mita 10,000 mwishoni mwa wiki jana.
Hata hivyo, maazimio hayo yalizimwa na Sifan Hassan wa Uholanzi na Letesenbet Gidey wa Ethiopia waliojitwalia dhahabu na fedha mtawalia.
Kenya ililazimika kuridhika na medali ya shaba iliyotwaliwa na Agnes Tirop.
Leo Obiri atakuwa na fursa ya kujinyanyua na kuendeleza ubabe wake hasa ikizingatiwa ubora wa rekodi ambayo amekuwa akijivunia katika kampeni nyingi za msimu huu.
Zaidi ya kushinda kivumbi cha kilomita 10 kwenye Mbio za Nyika za Dunia jijini Aarhus, Denmark mapema mwaka huu, Obiri pia alimaliza wa pili nyuma ya Tirop katika mbio za kitaifa za mita 10,000 jijini Nairobi mnamo Agosti.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Obiri, 29, kushiriki mbio za mita 10,000 katika ulingo wa kimataifa wiki iliyopita.
Licha kueleza kiwango cha kufadhaika kwake kwa kuambulia pakavu mwishoni mwa mbio hizo, anapigiwa upatu kujizolea dhahabu kirahisi hii leo na kushindia Kenya medali muhimu.
Obiri aliyeibuka wa kwanza katika mchujo wake wa Jumatano wiki hii kwa muda wa dakika 14:52.13, anajivunia muda bora zaidi wa dakika 14:20.36 katika kampeni za muhula huu. Muda wa kasi zaidi ambao amewahi kuusajili katika mbio hizi ni dakika 14:18.37.
Kasait aliambulia nafasi ya nne mchujoni kwa muda wa dakika 15:02.03. Atajibwaga ulingoni akijivunia hamasa tele baada ya kutawala mbio za mita 5,000 katika Michezo ya Afrika (AAG) iliyoandaliwa jijini Rabat, Morocco mwishoni mwa Agosti 2019.
Alifika utepeni akiwa wa kwanza baada ya muda wa dakika 15:33.63.
Mshindi huyu wa nishani ya shaba katika mbio za Nyika Duniani mnamo 2017 aliwaonyesha vumbi Waethiopia Feysa Hawi na Tariku Alemitu walioandikisha muda wa dakika 15:33.99 na 15:37.15 mtawalia.
Chelimo alitawazwa malkia wa Afrika katika mbio hizo jijini Brazzaville, Congo mnamo 2015.
Alikamilisha mchujo wake wa Jumatano katika nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 15:01.58.
Mbali na Mjerumani Konstanze Klosterhalfen na Elinor Purrier wa Amerika, baadhi ya wanariadha wanaotazamiwa kuwatoa Wakenya kijasho katika mbio hizi ni Waethiopia Hawi, Gemechu na Worku.