• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Tusker ngangari kuwa ngome imara ya wanasoka chipukizi

Tusker ngangari kuwa ngome imara ya wanasoka chipukizi

Na CHRIS ADUNGO

MBALI na kukisuka upya kikosi chao cha kwanza, Tusker FC ambao ni mabingwa mara 11 wa Ligi Kuu ya soka ya Kenya, wamefichua azma ya kuboresha timu yao ya chipukizi itakayoshiriki Ligi ya Divisheni ya Pili ya Shirikisho la Soka (FKF) Zoni ya Mashariki msimu ujao.

Mwenyekiti wa Tusker, Daniel Aduda, amesema kwa sasa wanaazimia kusajili idadi kubwa ya chipukizi na kuwadumisha wote waliotia fora katika miaka ya awali kadri wanavyojitahidi kuwapokeza malezi bora ya soka kisha kuwakweza hadi kikosi cha kwanza cha watu wazima.

Kwa mujibu wa Aduda, Tusker inapania kuwa ngome ya chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa talanta ambazo zitachangia kuimarika pakubwa kwa makali ya timu ya taifa ya Harambee Stars na kuboreka kwa viwango vya ushindani katika ligi ya soka ya Kenya.

Msimu jana, Tusker ambao wanalenga kusajili wanasoka wawili wa haiba kubwa kwa minajili ya kampeni zijazo, waliwakweza chipukizi Eric Zakayo na Mario Kakai hadi kikosi cha kwanza ambacho kwa sasa kinanolewa na mkufunzi Robert Matano.

Aduda ni miongoni mwa vinara wa soka ya humu nchini ambao wamechangamkia dili ya udhamini kati ya FKF na kampuni ya mchezo wa kamari ya Betking kutoka Nigeria.

Mbali na kudhamini soka ya Ligi Kuu ya Kenya kwa Sh1.2 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, BetKing pia imefadhili soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza kwa Sh100 milioni. Mpango huo utaendeshwa kwa miaka mitano ijayo huku kila kikosi kitakachoshiriki kivumbi hicho kikipokezwa Sh500,000 kwa mwaka.

“Hii ni mara ya kwanza katika historia ambapo soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza nchini Kenya imepata mdhamini. Ni hatua kubwa katika maendeleo ya soka yetu pamoja na makuzi ya thamani yake,” akasema Aduda.

Kufaulu kwa mpango huo wa udhamini kunamaanisha kwamba washiriki wote wa madaraja matatu ya soka ya Kenya wanafadhiliwa na kampuni za mchezo wa kamari. Kampuni ya Betika ndiyo inadhamini Ligi ya Kitaifa ya Daraja la Pili (NSL) huku Odibets ikifadhili ligi za soka ya mashinani.

You can share this post!

Vyakula vinavyoweza kuwasaidia wagonjwa wa kisukari

EPL: Aubameyang aongoza Arsenal kuwateremsha Watford daraja

adminleo