• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Tusker wamsajili beki wa haiba kutoka AFC Leopards

Tusker wamsajili beki wa haiba kutoka AFC Leopards

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 11 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Tusker, wamekamilisha usajili wa beki matata wa AFC Leopards, Christopher Oruchum.

Oruchum anakuwa mchezaji wa kwanza kuingia katika sajili rasmi ya Tusker baada ya kutia saini kandarasi ya miaka miwili.

Difenda huyo aliyejiunga na Leopards miaka miwili iliyopita kutoka Thika United kwa mkataba wa miaka minne, aliagana rasmi na Ingwe baada ya mkataba wake na Tusker ya kocha Robert Matano kutamatika.

“Tusker ni miongoni mwa klabu za haiba kubwa zaidi katika soka ya humu nchini na bara Afrika. Natarajia kunyanyua mataji zaidi nikiwa mwanasoka wa kikosi hiki,” akatanguliza Oruchum.

“Ni matumaini yangu kwamba nitaleta kitu cha kuthaminiwa zaidi ndani ya kikosi cha Tusekr ambacho kimeshuhudia ukame wa mataji katika kipindi cha misimu kadhaa iliyopita,” akasema.

“Nilikuwa pua na mdomo kusajiliwa na Tusker kutoka Thika United ila uhamisho huo ukatibuliwa katika dakika za mwisho baada ya AFC Leopards kuafikiana na wakala wangu mnamo 2018,” akaongeza Oruchum.

Kufikia sasa, Tusker tayari wamepoteza huduma za mshambuliaji mahiri Timothy Otieno aliyeyoyomea Zambia mwezi jana kuvalia jezi za Napsa Stars.

Mwenyekiti wa Tusker FC, Daniel Aduda, amesema hawatamsajili mwanasoka atakayeziba pengo la Otieno.

Badala yake, amefichua mipango ya kuwakweza ngazi mafowadi wawili kutoka kambi yao ya chipukizi ili kushirikiana vilivyo na washambuliaji Henry Meja na David Majak wa Sudan Kusini katika kampeni za msimu mpya wa 2020-21.

“Tuna idadi ya kutosha ya washambuliaji na viungo wavamizi. Kuna wanasoka wawili tutakaowasajili muhula huu, lakini ni beki na kiungo mkabaji. Mpango wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Otieno utakuwa wa baadaye, labda wa msimu ujao,” akasema Aduda katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Kauli yake ilishadidiwa na meneja wa timu, George Opondo ambaye amethibitisha kwamba tayari wamewakweza makinda Eric Zakayo na Mario Kakai hadi kikosi cha kwanza ambacho kwa sasa kinanolewa na mkufunzi Matano.

“Tusker ni ngome ya chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji ambavyo vitategemewa na kikosi cha chetu cha watu wazima na kile cha Ligi ya Divisheni ya Pili ya Shirikisho la Soka (FKF) Zoni ya Mashariki msimu ujao,” akasema Opondo.

Otieno ambaye pia ni mfumaji wa Harambee Stars, tayari ametia saini mkataba wa miaka miwili kambini mwa Napsa ambao pia wanajivunia huduma za kipa wa zamani wa Gor Mahia, Shaban Odhoji aliyejiunga nao msimu uliopita.

Tusker pia wamekatiza uhusiano na kipa mahiri mzawa wa Rwanda, Emery Mvuyekure, 30, ambaye kwa sasa yuko pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Katika msimu wa 2019-20, Otieno aliyejiunga na Tusker mnamo 2017 baada ya kujiengua kambini mwa Gor Mahia, alipachika wavuni jumla ya mabao 15 yaliyomweka kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa KPL. Nyota huyu aliyekuwa akihusishwa pakubwa na Wazito FC, aliwahi pia kuchezea Posta Rangers.

“Napsa walinipa ofa nzuri zaidi kuliko ile niliyokuwa nayo Tusker. Isitoshe, kikubwa zaidi kilichonishawishi kujiunga nao ni fursa ya kunogesha kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu ujao,” akatanguliza.

“Maamuzi ya kujiunga na Napsa yalikuwa rahisi kufanya licha ya kwamba nilisadikishwa pia na Odhoji ambaye aliwahi kucheza nami kambini mwa Gor Mahia,” akaongeza.

Kwa kutua Napsa ambao pia wanatazamiwa kusajili upya wanasoka Musa Mohammed na Duncan Odhiambo, Otieno anaungana na zaidi ya Wakenya 10 ambao kwa sasa wananogesha Ligi Kuu ya Zambia (ZSL).

Miongoni mwa masogora hao ni David ‘Calabar’ Owino, Jesse Jackson Were (wote wa Zesco United); John Mark Makwatta (Buildcon FC); Ian Otieno, Andrew Tololwa (Red Arrows), Ismail Dunga, Shaban Odhoji (wote wa Napsa Stars), Harun Shakava, Duke Abuya (wote wa Nkana FC).

Tusker wamethibitisha pia kukamilisha shughuli za kuukarabati uwanja wao wa nyumbani wa Ruaraka ambao kwa sasa umewekewa zulia jipya la kisasa.

Aduda amesema kwamba wanashughulikia sasa pia mifereji ya majitaka katika jitihada za kurejesha na kudumisha usafi na hadhi ya uwanja huo ambao umekuwa katika hali mbaya kwa kipindi kirefu.

“Licha ya uchechefu wa fedha unaotukabili kwa sasa, kikosi kimepania kuchuma nafuu kutokana na janga la corona na kukarabati uwanja chini ya uelekezi wa Wycliffe Omondi anayesimamia masuala ya uga wa Ruaraka,” akasema Aduda.

Viongozi wa Tusker na wa Kamati ya KPL ya Viwanja na Usalama wamekuwa wakikashifiwa pakubwa kwa kuidhinisha mechi mbalimbali kusakatiwa ugani Ruaraka licha ya hali duni ya uwanja huo.

Mbali na kutumiwa kuandalia michuano mbalimbali ya KPL, uwanja wa Ruaraka umekuwa pia mwenyeji wa mapambano ya Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza (NSL) na gozi la Betway Shield Cup katika msimu wa 2019-20.

Baada ya uwanja huo kukarabatiwa, ipo mipango ya shughuli za ujenzi wa maeneo ya wageni rasmi na mashabiki pia kukalia. Hili ni jambo ambalo Aduda ameshikilia kwamba litaupa uga wa Ruaraka sura mpya kwa mujibu wa viwango bora vya kimataifa vinavyohitajika.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya vivumishi...

AK yafutilia mbali majaribio ya mbio kwa minajili ya...