Twaha Mbarak atangaza kuwania kiti cha urais FKF
Na JOHN ASHIHUNDU
NAIBU mwenyekiti wa klabu ya Bandari FC, Twaha Mbarak, amejitupa uwanjani kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi ujao wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF).
Akitangaza manifesto yake Jumanne, Twaha alitoa wito kwa Serikali ihakikishe kila wahusika wameshiriki kwenye kura hizo kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo hatua ya watu kadhaa kufungiwa nje ilichangia kuibuka kwa makundi mawili yaliyoleta mgawanyika mkubwa katika uongozi wa mchezo huo.
“Lengo langu ni kuimarisha kandanda kuanzia mashinani na kuhakikisha wachezaji bora wanapatikana ili kupewa nafasi katika vikozi vya timu za kitaifa. Niko tayari kushirikiana na washikajidau katika juhudi za kuhakikisha timu zetu zinafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa,” alisema katika taarifa yake.
“Nikifanikiwa kutwaa uongozi, nitateua kamati mpya ya kiufundi itakayoleta mawazo mapya ya kuimarisha timu zetu za taifa. Kamati itakayokuwa na utaratibu bora kuanzia kwa timu za vijana hadi juu,” aliongeza.
Twaha alisema afisi yake itahakikisha waamuzi wa soka wanapata mafunzo yanayofaa ili wapate fursa ya kusimamia mechi kubwa kote Duniani.
“Tuko na mipango ya kuimarisha viwango vya makocha, waamuzi pamoja na wasimamizi wengine wa mchezo huu kwa jumla.”
Alisema atahakikisha Kenya inapata watu walio na mafunzo ya juu ya usimamizi wa mchezo huu, mbali na kutafuta wafadhili watakaohakikisha mechi za ligi zinaonyeshwa moja kwa moja katika runinga.
“Tutashirikiana na Kaunti zote 47 pamoja na kampuni zenye uwezo wa kudhamini soka katika viwango vyote kuanzia mashinani na kuhakikisha kuna haki na ukweli katika matumizi yetu ya kifedha,” aliongeza.
Twaha alisema atahakikisha Kenya ina uhusiano mwema na mataifa ya kigeni yaliyopiga hatua kubwa katika mchezo huu.
“Tutakuwa na uhusiano wa karibu na Shiriksiho la Kimataifa la Soka (FIFA), Chama cha Soka Afrika (CAF) pamoja na Shirikisho la Kandanda Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Kwenye kikao cha FKF kilichofanyika wikendi iliyopita, shirikisho hilo lilitoa masharti kadhaa yatakayoangaliwa kabla ya mtu kuruhusiwa kuwania kiti.
Miongoni mwa masharti hayo ni Sh300,000 kwa yeyote anayetaka kuwania kiti cha juu, mbali na kuhakikisha ana rekodi nzuri pamoja na stakabadhi muhimu za kusafiria.
Mbali na Twaha, wengine waliotangaza kuwania kiti cha urais ni MacDonald Mariga, Hussein Mohammed, Sam Nyameya, Sammy Owino, Robert Macharis na Sam Ocholla.