Ubabe uliotarajiwa kati ya Kiptum na Kipchoge katika 42km wazimwa na kifo cha ghafla
Na GEOFFREY ANENE
VITA vya ubabe vilivyotarajiwa kwa hamu kubwa kwenye mbio za kilomita 42 kati ya Wakenya Eliud Kipchoge na Kelvin Kiptum havitashuhudiwa kufuatia kifo cha Kiptum katika ajali mbaya ya barabarani Jumapili usiku.
Kipchoge, 39, na Kiptum, 24, walitiwa katika kikosi cha Kenya cha marathon kitakachoshiriki Michezo ya Olimpiki mwezi Julai/Agosti jijini Paris, Ufaransa mwaka huu.
Wakenya hao wawili hawakuwa wamekutana katika mashindano na mashabiki walikuwa wakisubiri kwa hamu kuona itakavyokuwa jijini Paris.
Kiptum alifuta binadamu wa kwanza kukamilisha mbio rasmi za 42km chini ya saa mbili na dakika moja baada ya kushinda Chicago Marathon kwa saa 2:00:35 mwezi Oktoba mwaka 2023.
Alifuta rekodi ya Kipchoge ya 2:01:09 ambayo ilikuwa imewekwa Septemba mwaka 2022 jijini Berlin, Ujerumani.
Kiptum alikuwa tayari ameanza kubatizwa kuwa ndiye mfalme mpya wa mbio za 42km baada ya kutawala Valencia Marathon nchini Uhispania kwa 2:01:53 mnamo Desemba 2022, London Marathon kwa 2:01:25 (Aprili 2023) na Chicago Marathon (Oktoba 2023).
Kifo chake kimetokea miezi michache baada ya kutawazwa Mwanariadha Bora Duniani wa mbio ndefu mwaka 2023 mwezi Desemba. Rekodi yake ya dunia ya 2:00:35 pia ilirasimishwa siku chache zilizopita.
Kiptum ameaga dunia pamoja na kocha wake Gervais Hazimana kutoka Rwanda. Alikuwa anajiandaa kufungua msimu kwa kutimka Rotterdam Marathon nchini Uholanzi hapo Aprili 14, akilenga kuimarisha rekodi yake ya dunia.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Marakwet Peter Mulinge, Kiptum alikuwa anaendesha gari aina ya Toyota Premio, akiwa na Garvais na mwanamke aliyetambuliwa kama Sharon Kosgey, wakielekea nyumbani kutoka Eldoret wakati gari lake lilitoka barabarani na kugonga mti katika eneo la Kaptagat.
Sharon aliponea kifo, lakini akiwa na majeraha mabaya. Alikimbizwa katika hospitali ya Racecourse, huku miili ya Kiptum na Garvais ikapelekwa mochari ya hospitali hiyo.
Uchunguzi ungali unaendelea kuhusu kilichosababisha ajali hiyo.