Michezo

Ubelgiji roho mkononi, Ureno wakimezea kutua kileleni kundi lao Euro 2024

Na MASHIRIKA June 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

STUTTGART, UJERUMANI

MECHI za makundi katika michuano ya Euro 2024 zinamalizika leo usiku huku pambano kali likitarajiwa kuwa kati ya Ubelgiji na Ukraine, timu zote mbili zikihitaji ushindi ili kutinga hatua ya 16-bora.

Kila timu katika kundi hili la E imeshinda mechi moja na kushindwa pia mara moja.

Romania iko kileleni kutokana na ubora wa mabao.

Ubelgiji wanakamata nafasi ya pili mbele ya Slovakia na Ukraine baada ya kila moja kucheza mara mbili.

Katika mechi ya leo, Ubelgiji haina namna nyingine zaidi ila kushinda Ukraine ili ifuzu.

Kikosi hicho cha kocha Domenico Tedesco ni miongoni mwa timu zinazowekewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa mwaka huu.

Lakini kinatarajiwa kupitia katika hali ngumu kutokana na ukuta mgumu wa Ukraine inayojumuisha Oleksandr Zinchenko, Vitaliy Mykolenko, Illia Zabarny na Andry Yarmolenko.

Ubelgiji ilianza vibaya kwa kushindwa kwa bao 1-0 na Slovakia kabla ya kurejea kwa kishindo na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Romania.

Ukraine kwa upande wake ilianza kwa kuchapwa 3-0 na Romania kabla ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Slovakia katika mechi iliyofuata.

Ubelgiji wanataka kumaliza kinara kwenye kundi hili, ili kucheza na timu itakayokuwa imeshika nafasi ya pili katika Kundi F linaloongozwa na Ureno.

Endapo watamaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo, huenda wakacheza na Ureno kwenye hatua ya 16-bora.

Uturuki wanakamata nafasi ya pili kwa alama tatu huku Jamhuri ya Czech na Georgia wakikung’uta mkia kwa alama moja kila mmoja.

Kwingineko, Georgia watacheza na Ureno ambayo tayari imetinga hatua hiyo ya 16-bora, lakini wanahitaji ushindi au sare ndipo wamalize kileleni.

Cezch ambayo itakabiliana na Uturuki imekuwa ikijaribu kwa miaka mingi kubeba taji hili bila mafanikio.

Hesabu zinavyoonekana, inawezekana timu hiyo ikamaliza katika nafasi ya tatu.

Matumaini yao ya kusonga mbele na kuingia 16-bora yatategemea jinsi mechi nyingine za kundi hili zitakavyokwenda.