Michezo

Ubelgiji wazima ndoto ya Uingereza kushiriki fainali za UEFA Nations League mwaka huu

November 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

UINGEREZA hawatashiriki fainali za UEFA Nations League mwaka huu baada ya matumaini yao finyu kuzimwa na Ubelgiji waliowapokeza kichapo cha 2-0 mjini Leuven mnamo Novemba 15, 2020.

Japo wanasoka wa kocha Gareth Southgate walimiliki asilimia kubwa ya mpira dhidi ya Ubelgiji ambao kwa sasa wanaorodheshwa wa kwanza kimataifa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Uingereza walitepetea katika safu ya mbele na wakazamishwa na mabao ya mapema yaliyofumwa wavuni na Youri Tielemans na Dries Mertens.

Wawili hao walishirikiana vilivyo na Kevin de Bruyne na Romelu Lukaku aliyepoteza nafasi nyingi za wazi. Ina maana kwamba Uingereza hawatashiriki fainali ya Nations League kwa mara nyingine baada ya kuambulia nafasi ya tatu katika makala ya kwanza yaliyotawaliwa na Ureno mnamo 2019.

Katika mechi nyingine ya Kundi A2, kiungo Christien Eriksen wa Inter Milan alifunga mabao mawili na kuwapa Denmark ushindi muhimu wa 2-1 dhidi ya Iceland. Uingereza kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama saba, tano nyuma ya viongozi Ubelgiji. Denmark ni wa pili kwa alama 10 huku Iceland wakikokota mkia bila pointi.

Pigo zaidi kwa Uingereza waliokosa huduma za Marcus Rashford na Raheem Sterling dhidi ya Ubelgiji ni kuumia kwa kiungo Jordan Henderson beki sajili mpya wa Chelsea, Ben Chilwell. Kutokuwepo kwa Sterling kulimpa Southgate fursa ya kutegemea maarifa ya kiungo matata wa Aston Villa, Jack Grealish.

“Ilikuwa mechi ngumu kwetu baada ya Ubelgiji kufunga mabao mawili ya haraka katika kipindi cha kwanza. Kukosekana kwa Sterling na Rashford pia kulituathiri kwa kuwa tulikosa kasi katika safu ya mbele,” akasema Southgate.

Kwa upande wake, kocha Roberto Martinez wa Ubelgiji alikuwa mwingi wa sifa kwa wachezaji wake, akisisitiza kwamba ushindi dhidi ya Uingereza utawapa motisha zaidi ya kuangusha Denmark mnamo Novemba 18, 2020. Uingereza watakuwa pia wenyeji wa Iceland siku hiyo.

Uingereza waliopigwa 1-0 na Denmark mnamo Oktoba 14, kwa sasa wamepoteza mechi mbili mfululizo za kimataifa kwa mara ya kwanza tangu Septemba 2018 walipocharazwa tena na Ubelgiji kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.

Kichapo ambacho Uingereza walipokezwa kilikuwa cha 10 kutokana na mechi 48 ambazo zimesimamiwa na Southgate. Sasa anakuwa kocha wa pili wa Uingereza kuwahi kupoteza michuano 10 tangu Sven-Goran Eriksson apoteza idadi sawa na hiyo ya mechi kati ya 67 alizozisimamia.

Hadi walipoangushwa na Uingereza (2-1) mnamo Oktoba 11, Ubelgiji hawakuwa wamepoteza mchuano wowote katika mashindano yote tangu wapokezwe kichapo cha 5-2 kutoka kwa Uswisi kwenye Nations League mnamo 2018-19. Ilikuwa mara ya pili kwa Uingereza kuwapiga Ubelgiji tangu wavune ushindi wa 1-0 katika hatua ya 16-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 1990.

Ushindi uliosajiliwa na Ubelgiji katika mechi 12 kati ya 13 mfululizo ulichangia pakubwa kupaa kwao hadi kileleni mwa orodha ya FIFA.

Ubelgiji waliingia katika mchuano wa Novemba 15 dhidi ya Uingereza wakipania pia kuendeleza ubabe ambao uliwavunia ushindi wa 2-1 dhidi ya Iceland kwenye gozi lililopita la Nations League mnamo Oktoba 14 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Uswisi katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha jijini Brussels mnamo Novemba 11.

Kwa upande wao, Uingereza walikuwa na kiu ya kujinyanyua kwenye Nations League baada ya chombo chao kuzamishwa na Denmark kwa kichapo cha 1-0 mnamo Oktoba 14. Isitoshe, walikuwa wakijivunia ari tele kutokana na ushindi wa 3-0 waliousajili dhidi ya Jamhuri ya Ireland kirafiki Novemba 12.

Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Uingereza ya kocha Gareth Southgate kuwahi kusajili dhidi ya Ireland tangu 1985. Mabao yao yalipachikwa wavuni kupitia Harry Maguire, Jadon Sancho na Dominic Calvert-Lewin.

Kilichowapa Uingereza msukumo zaidi ni tija ya kulaza Ubelgiji mara mbili mfululizo baada ya masogora hao wa Martinez kuwapiga pia mara mbili kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

Baada ya kuwapepeta Uingereza 1-0 kwenye mojawapo ya mechi za makundi mnamo 2018, Ubelgiji walizamisha chombo cha Uingereza kwa mabao 2-0 kwenye gozi la kuamua mshindi wa nafasi ya tatu baada ya kabla ya Ufaransa kuwabwaga Croatia kwa 4-2 kwenye fainali.