• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ubelgiji yaminya Waskochi huku Brazil wakila hu!

Ubelgiji yaminya Waskochi huku Brazil wakila hu!

Na MASHIRIKA

GLASGOW, Scotland

KIUNGO mahiri Kevin de Bruyne aling’ara na kuisaidia Ubelgiji kuibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Scotland katika mechi ya mchujo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Euro 2020.

Staa huyo wa Manchester City aliwaandalia pasi Romelu Lukaku, Thomas Vermaelen na Toby Alderweireld zilizosababisha mabao matatu kabla ya mwenyewe kufunga la nne

Matokeo hayo yalikuwa mabaya kwa Scotland ya kocha Steve Clarke, kwani huenda wakalamizika kushiriki mechi ya mchujo baada ya mechi za makundi kumalizika. Scotland imesubiri kwa kipindi cha miaka 22 bila kushiriki katika michuano yoyote mikubwa.

Kwa upande mwingine, ulikuwa ushindi wa sita katika mechi sita kwa Ubelgiji chini ya Roberto Martinez, ambao wanaongoza Kundi A.

Mbali na kushinda mechi hiyo iliyochezewa Hampden, Ubelgiji walicheza soka ya kuvutia kuthibitisha nafasi yao ya kwanza duniani katika viwango vya kimataifa.

Scotland, inayoshikilia nafasi ya tano, kwa sasa ipo nyuma ya Urusi kwa tofauti ya pointi tisa, na Ubelgiji kwa tofauti ya alama 12, huku zikiwa zimebaki mechi nne za kundi hilo.

Kwingineko, rekodi ya Brazil kutoshindwa ya mechi 17 hatimaye imezimwa na Peru ambao waliwachapa 1-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezewa Los Angeles.

Afunga bao muhimu

Luis Abram alifunga bao hilo muhimu dakika ya 84, kikiwa kichapo cha kwanza kwa mabingwa hao mara tano wa Dunia katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

Kuingizwa kwa Neymar, Vinicius Junior, Lucas Paqueta na Bruno Henrique katika kipindi cha pili haukuzaa matunda kama ilivyotarajiwa. Ilikuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana baada ya Brazil kuibuka na ushindi wa 3-1 katika fainali ya Copa America mwezi Julai.

Katika mechi nyingine, mshambuliaji Lautaro Martinez wa Inter Milan alifunga mabao matatu katika ushindi wa Argentina wa 4-0 dhidi ya Mexico katika pambano la kupimana nguvu lililochezewa San Antonio.

Bao jingine lilifungwa na kiungo Leandro Paredes Paris St-Germain aliyefunga kupitia kwa mkwaju wa penalti.

  • Tags

You can share this post!

RONALDO MUUAJI! Ureno yaipiga Lithuania 5-1

Southgate akiri kukamwa kijasho vilivyo na Kosovo

adminleo