Michezo

UBINGWA EPL: Kazi bado ipo

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu nchini hapa ni kali mno kuliko wakati mwingine ule.

Mkufunzi huyo amesema kasi inayoonyeshwa na klabu nne kubwa kwenye ligi hiyo imeshangaza kila mtu, wala sio yeye pekee.

Guardiola amesema vita hivyo ni vya mafahali watano, Liverpool, Manchester City, Chelsea, Arsenal na Tottenham.

“Vita vya ubingwa wa msimu huu ni vya vigogo watano, nasema hili nikiwa najiamini,” alisema kocha huyo wa zamani wa klabu ya Bayern Munich na FC Barcelona.

“Ukiangalia vizuri msimamo ulivyo, hakuna tofauti kubwa sana ya pointi kati ya timu tano au sita zinazofuatana, ikiwemo Tottenham ambayo daima imekuwa ikitoa upinzani mkali kwa zile nne bora,” alisema Guardiola.

Mashabiki wameshuhudia matokeo ya kushangaza ikilinganishwa na ilivyokuwa msimu uliopita wakati kama huu baada ya kila timu kucheza mechi 10.

Liverpool na Everton ni miongoni mwa timu zinazoendelea kupata matokeo ya ushindi kuliko zilivyokuwa msimu uliopita, lakini hali imekuwa ngumu kwa Manchester United ambao msimu uliopita kufikia wakati kama huu walikuwa moto wa kuotea mbali.

Wakati kikosi hicho cha kocha Jose Mourinho kikiendelea kutatizika, wapinzani wao wakuu, Manchester City wameendeleza ubabe wao ambapo kufikia sasa hawajashindwa.

Kimekuwa kibarua kigumu kwa timu zote tatu zilizojiunga na ligi hiyo maarufu.

Wolves ilichapwa 1-0 na Brighton licha ya mwanzo wao mzuri msimu huu, huku Cardiff ikibwagwa 4-1 na Liverpool.

Hali imekuwa ngumu kwa Newcastle United ambao imekuwa vigumu kufunga mabao wala kuzuia kufungwa.

Huddersfield wamekuwa wakipokezwa vichapo mara kwa mara, wakati Manchester United ikiwa katika nafasi ya nane.

Southampton ambao walikaribia kushuka daraja msimu uliopita pia wameanza vibaya msimu huu.

Wengi wanawawekea Manchester City nafasi kubwa ya kuhifadhi ubingwa, lakini makali yao ya msimu uliopita yanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Liverpool na Chelsea.

Ukame wa mabao wa Crystal Palace chini ya kocha Roy Hodgson ulimalizika walipofanikiwa kufunga dhidi ya Arsenal, lakini lazima waendelee kupata ushindi katika mechi zijazo ili waepuke masaibu ya msimu uliopita.

West Ham wamepitia katika hali ngumu kutokana na majeraha kwa nyota wao kadhaa, lakini wamejitahidi vilivyo kubakia katika nafasi nzuri ya kubakia ligini msimu ujao.

Leicester chini ya Claude Puel imeonyesha dalili nzuri na huenda ikaendelea kuvuma hata baada ya kumpoteza mmiliki wake Vichai Srivaddanaprabha aliyefariki kwenye ajali ya ndege juma lililopita.

Tottenham imeanza msimu kwa kishindo, ingawa mapema juma hili walichapwa 1-0 na Manchester City ugani Wembley.

Hata baada ya rekodi yao ya ushindi kuzimwa mwishoni mwa wiki, Arsenal wameanza kurejea katika hali yao nzuri tangu wapate kocha mpya, Emery Unai.

Watford wamekuwa wakipata matokeo ya kuchanganya tangu msimu uanze na itabidi wajitahidi.

Kwingineko, kocha Maurizio Sarri hana presa kutokana na matokeo mazuri yanayofuatana msimu huu tangu klabu hiyo iagane na Antonio Conte.

Everton walianza vibaya, lakini kocha Marco Silva amepata mfumo unaofaa.