Michezo

Ubingwa wa mapema waisubiri Kinyago

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kinyago United inazidi kutesa wala haitingiki kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa wa Ligi ya KYSD muhula huu.

Chipukizi hao wanazidi kufyeka wapinzani wao kwenye kinyang’anyiro hicho kinaoshirikisha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14.

Kinyago United chini ya nahodha, Samuel Ndonye inazidi kuzua msisimko wa kufa mtu ambapo imefanikiwa kushinda mechi zote 12 ambazo imeshiriki.

”Hatutaki kujipatia ubingwa wa mapema lakini nashukuru vijana wangu wanaendelea kujituma kiume kuashiria wazi hawataki masihara huku wakilenga kufanya kweli dhidi ya wapinzani wao,” anasema kocha wake, Anthony Maina na kuongeza kuwa wanatarajia kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo mbele ya washiriki wengine kwenye michuano ya msimu huu.

Anadokeza kuwa ana imani wapinzani wao wanapania kujipanga kivingine kwenye mechi za mkumbo wa pili. Anadai kuwa Young Achievers kati ya vikosi vilivyotazamiwa kuzua ushindani mkali kwa vijana wake kiasi ilijaribu kuzima ndoto yao kabla ya kuteleza na kuilaza mabao 3-0.

Hata hivyo alikiri kuwa hatuna timu wanazodharau kwa kuzingatia vikosi vyote vinazidi kupigana kwa udi na uvumba kwenye kampeni za muhula huu.

Ili kukamilisha michezo ya mkombo wa kwanza Kinyago United imeratibiwa kucheza dhidi ya Gravo Legends, Sharp Boys, State Rangers kisha kupepetana na Fearless Academy.

Kocha huyo anaamini kuwa endapo wachezaji wake watamaliza raundi ya kwanza wakiwa kifua mbele watakuwa wamejiweka pazuri kuhifadhi taji hilo na kulishinda kwa mara ya 13.

Baada ya kipute hicho kukunjua jamvi kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo alinukuwa akisema “Bila kujipigia debe kampeni za muhula huu zinatarajiwa kuzua ushindani mkali maana timu zote zimejipanga kukabiliana kwa udi na uvumba.”

Sharp Boys ambayo imeshiriki mechi kumi inashikilia nne bora wa kuzoa alama 21 ilhali Kinyago United ingali kileleni kwa alama 33. Timu zingine zinazojituma kwenye kampeni hizo ni Volcano FC na Fearless FC bila sahau MASA inayofunga tano bora kwa alama 22 kutokana na mechi 12.

Kwenye ngarambe ya muhula uliyopita, Kinyago ilihifadhi ubingwa huo kwa kuzoa alama 57, tatu mbele ya MASA. Vile vile ilijivunia kutawazwa mabingwa wa timu zilizomaliza kati ya nane bora (Top Eight).

Fernabache iliyokuwa ikipigiwa chapuo kutwaa taji hilo iliibuka tatu bora kwa kuzoa pointi 51 ilipoteleza na kulazwa mabao 2-1 na Locomotive FC kwenye mechi ya mwisho.

Kinyago inajumuisha: Peter Gathuri, Newton Maina, Alvin Muteti, Abednego Wawire, Abdallah Shame, Alphonse Ndungu, Thierry Henry, Boniface Ariemba na Samuel Ndonye (nahodha).

Pia wapo Jahason Wakachala, Austine Okoth, Iphrahim Oyando, Samuel Kamau, Chrisphine Mamwacha, Titus Muimi, Peter Waweru, Collins Juma na Daniel Mwangi.