Michezo

Uchaguzi wa ofisi mpya FKF wapigwa breki

December 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

JOPO la Malalamishi ya Spoti (SDT) limefutilia mbali uchaguzi wa kitaifa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) uliokuwa ufanyike wikendi hii.

Katika uamuzi uliotolewa Jumanne na mwenyekiti wa jopo hilo John Ohaga, FKF kwa sasa italazimika kuanza upya mchakato wa kuandaa uchaguzi mpya kwani pia matokeo ya uchaguzi wa maeneo, uliofanyika Novemba 23, yametupiliwa mbali.

Kulingana na Ohaga, uchaguzi huo wa kitaifa ulifutiliwa mbali kwa sababu umma haukushirikishwa vilivyo jinsi inavyoagiza kanuni za uchaguzi za FKF.

Kura hiyo ilikuwa imepangiwa kufanyika Jumamosi hii katika uwanja wa Kasarani mjini Nairobi.

Aidha, waliokuwa wawaniaji wengine wa urais wa FKF, ikiwemo Sam Nyamweya, Alex Ole Magelo, Steve Mburu na Moses Akaranga, walikuwa wamelalamikia hatua ya kuwafungia nje ya kura hiyo.

Wanne hao walitilia shaka uhalali wa Bodi ya Uchaguzi ya FKF chini ya Mwenyekiti Edwin Wamukoya, wakidai haikubuniwa kwa mujibu wa sheria.

“Tumefutilia mbali matokeo ya chaguzi zote za awali, na kuahirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi wa kitaifa uliokuwa ufanyike wikendi hii,” akasema Ohaga katika uamuzi huo.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Rais wa FKF Nick Mwendwa alisema watapanga uchaguzi mwingine kufikia Aprili 2020 chini ya kanuni na sheria zote zilizopo.

“Tutawaalika wajumbe wote kwa kikao ili kujadili upya mchakato wa uchaguzi, ambao utaandaliwa kufikia mwisho wa Aprili 2020,” akasema.

Uchaguzi huo wa wikendi hii ulikuwa usimamiwe na Afisa wa Idara ya Utawala wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Sara Solemale ambaye alitarajiwa kuwasili nchini Ijumaa.

Jumla ya wajumbe 94 kutoka kila kaunti, Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Betika Super League, Ligi ya Daraja ya Pili (FKF Division One) na Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) walitarajiwa kupiga kura katika uchaguz huo.

Rais Nick Mwendwa, naibu wake Doris Petra na wanachama wengine wanane wa Kamati Kuu ya FKF (NEC), watatetea nyadhifa zao kwa muhula mwingine wa miaka minne ofisini.

Kufikia Jumanne maafisa wote wa sasa wa FKF hawakuwa na wapinzani katika uchaguzi huo wa wikendi.

Wakati huo huo, Sally Bolo, Kerubo Momanyi na Margaret Omondi walikuwa wakiwania wadhifa mpya wa Mwakilishi wa Kike katika Kamati Kuu (NEC).