• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Uchambuzi wa takwimu za mechi ya Tanzania dhidi ya Morocco

Uchambuzi wa takwimu za mechi ya Tanzania dhidi ya Morocco

NA MWANGI MUIRURI

TANZANIA ilianza vibaya mashindano ya taji la Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023) baada ya Morocco kuilambisha mabao matatu kwa nunge.

Vijana wa Taifa Stars kama wanavyofahamika, waliingia katika uwanja wa Stade de San Pedro nchini Cote d’Ivoire wakionekana wanyonge dhidi ya wenzao Atlas Lions wa Morocco.

Ingawa hivyo, takwimu zinaonyesha walicheza kwa kujituma ambapo Tanzania ilifanikiwa kupata asilimia 48 nayo Morocco ikipata 52, tofauti ya asilimia nne pekee ya umiliki wa mpira.

Tanzania ilianza kuzidiwa ujanja pale refa Al Hadi Allou Mahamat alimlisha Novatus Miroshi kadi nyekundu katika dakika ya 70 kwa kucheza ngware.

Morocco ambayo katika dakika ya 30 ya mchezo ilikuwa imepata bao kupitia beki wake wa katikati Romain Saiss, iliendelea kuishambulia Tanzania amapo Azedine Ounahi aliwaamsha tena mashabiki kupitia goli la dakika ya 77 naye Youssef En-Nesyri akafunga kazi kwa kutinga lingine kunako dakika ya 80.

Lakini licha ya masaibu hayo ya kupokezwa kichapo cha 3-0 na kufanya Afrika Mashariki kwa ujumla ionekane dhaifu katika dimba hilo linaloshirikisha mataifa 24, vijana hao wa kocha Andre Amrouche walionyesha mchezo wa kusakama mno, hali ambayo kwa upande mmoja iliwaponza kwa kadi.

Katika safu ya kutandaza pasi za kuonana, Morocco ilipata 465 nao Tanzania wakionana ugani guu hadi kwa guu kwa mara 449.

Shabaha ya pasi licha ya kuwa na upinzani wa timu ambayo imeorodheshwa ya 13 kwa ubora duniani, Tanzania ambayo ni ya 121 kwa ubora duniani ilijipa asilimia 83. Morocco ilipata ufasaha wa pasi wa asilimia 87, nne pekee juu ya Tanzania iliyokuwa na wachezaji 10.

Tanzania aidha ilifanikiwa kuelekeza mashuti mawili langoni mwa Morocco lakini hakuna lililolenga michuma. Lakini Morocco waliachilia fataki 14 ambapo saba zililenga langoni na tatu kwa hizo zikatikisa nyavu.

Tanzania ilipata kona mbili huku Morocco ikipata tano katika mechi ambayo hakuna aliyejenga kibanda kwa wenywewe bila idhini.

Tanzania iliwalemea Morocco kwa kucheza ngware ambapo hali iliishia 13-12 hali hiyo ikisababishia vijana hao wa Rais Samia Suluhu adhabu ya kandi tatu za manjano dhidi ya mbili za Morocco na kadi moja nyekundu dhidi ya sufuri.

Baada ya kila timu katika ‘Kundi F’ kucheza mechi moja moja, Morocco inaongoza kwa alama tatu ikiwa na ubora wa magoli matatu. Inafuatwa na DR Congo katika nafasi ya pili baada ya kutoka sare ya 1-1 na na Zambia inayokamata nafasi ya tatu kwa alama moja pia. Tanzania inashika mkia ikiwa na upungufu wa mabao matatu bila alama yoyote.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wito fedha za NG-CDF zimwagwe kwa miradi ya kubuni ajira

Bobi Wine awekwa ‘chini ya kizuizi’ nyumbani

T L