Michezo

UEFA: Kibarua cha ‘Ndovu’ Arsenal kulipuana na Porto saa tano usiku

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

LEO ni leo ikitinga saa tano usiku ambapo mashabiki wa Arsenal nchini Kenya watakuwa wameshika roho mkononi timu yao itakapovaana na FC Porto ya Ureno katika mchuano wa mkondo wa marudiano awamu ya 16-bora Klabu Bingwa Ulaya (Uefa).

Tayari, wafuasi wa ‘Ndovu’ Arsenal wameanza kupigiana simu wakutane katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumbi za burudani kushangilia timu hiyo yao na kuitakia ushindi dhidi ya vijana wa kocha Sergio Paulo Marceneiro da Conceicao.

Porto katika jedwali la ligi kuu Ureno iko katika nambari ya tatu ikiwa na pointi 46, hii ikiwa ni nyuma ya viongozi Sporting Lisbon (69) na nambari mbili Benfica (61).

Na katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Arsenal iko kidedea ikiwa na pointi 64, ikiitwa “Ndovu juu ya mti”.

Katika awamu ya kwanza ya michuano hiyo ya Uefa nchini Ureno mnamo Februari 1, 2024, Arsenal ilipigwa na butwaa kwa kupigwa goli 1-0 katika dakika ya 90+4 kutoka kwa guu la Wanderson Rodrigues do Nascimento Galeno,26, ambaye ni raia wa Brazil.

Leo Jumanne ikiwa ni zamu ya Arsenal kualika wageni ugani Emirates, ni lazima The Gunners washinde Porto kwa ubora wa mabao mawili, iwe ni 2-0, 3-1, 4-2, 5-3 ama hata 10-8.

Kinyume cha ushindi huo wa ubora wa magoli mawili ni Arsenal ipate ushindi wa ubora wa goli moja ndio kuwe na muda wa ziada na hatimaye mashuti ya penalti yaamue mshindi endapo timu hizo hazitakuwa zimefungana.

Kinyume na ushindi wa Arsenal katika hali hizo zote, ina maana kwamba itang’atuliwa kutoka kinyang’anyiro hicho katika awamu hiyo kutoka 16-bora na kwa siku kadha zijazo, mashabiki wake wakubali kejeli za mahasidi wao wakuu Manchester United, ambao kwa sasa katika jedwali la EPL, wako nyuma ya ‘Ndovu juu ya mti’ kwa pointi 17 baada ya wote wawili kucheza mechi 28 hadi sasa kati ya zote 38.

Huku Arsenal ikiwa na 46 kama ubora wa mabao, Man U wako na sufuri baada ya kuingiza magoli 39 na kupigwa magoli 39 pia.

Mkufunzi wa Arsenal Mikel Arteta tayari amekiri kwamba Jumanne usiku kuna mlima wa kukwea lakini akaahidi kwamba “mtashuhudia nguvu ugani Emirates ambazo hamujawahi kuziona maishani mwenu”.

“Kelele zitakuwa za kichaa na mazingara yatakuwa ya mauaji,” akasema kocha Arteta.

Licha ya ujasiri huo wa kocha, cha kutia wasiwasi ni kwamba, katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza dhidi ya Porto, Arsenal ilitawala umiliki wa mpira kwa asilimia 65 dhidi ya 35 lakini ikakosa hata shuti moja lililolenga michuma.

Porto ilipiga mashuti manane dhidi ya saba ya Arsenal na pasi zilizotandazwa zikiwa ni 495 za Arsenal na 274 za Porto. Uhakika wa pasi hizo ulikuwa asilimia 87 kwa manufaa ya Arsenal nayo Porto ikiwa na uhakika wa asilimia 75.

Huku Arsenal ikicheza ngware mara 22, Porto ilizicheza kwa kiwango cha 14 na katika hali hiyo, vijana hao wa Arteta wakapokezwa kadi tatu za manjano dhidi ya mbili za upande ule mwingine. Arsenal ilipata kona 10 huku Porto ikichanja kona moja.

[email protected]