Michezo

UG yatua nchini kupimana nguvu na Stars kesho Jumapili

September 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Uganda almaarufu Uganda Cranes iliwasili jijini Nairobi mnamo Ijumaa tayari kupima makali ya wenyeji Harambee Stars katika mechi ya kirafiki.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa makocha wapya Francis Kimanzi (Kenya) na Abdallah Mubiru (Uganda) tangu Wafaransa Sebastien Migne na Sebastien Desabre waondoke baada ya Kombe la Afrika (Afcon) lililokamilika nchini Misri wiki saba zilizopita.

Mubiru na vijana wake waliwasili mapema Ijumaa kwa mechi hiyo itakayosakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani mnamo Jumapili saa kumi jioni.

Majirani hao wa Kenya watapata fursa ya kuutumia uwanja wa Kasarani kwa mazoezi leo jioni. Stars imekuwa ikifanyia mazoezi yake uwanjani humu tangu Jumatatu.

Timu zote mbili zitatumia wachezaji wao wakali katika kipindi hiki cha mechi za mataifa cha Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Uganda, kwa mfano, ina wachezaji matata kama Luwagga Kizito (Kazakhstan) na Aucho Khalid, Emmanuel Okwi, Lwanga Taddeo na Allan Kyambadde (wote wa Misri).

Kimanzi, ambaye amerejea kuongoza Stars kwa mara ya tatu, amepata huduma za washambuliaji Michael Olunga (Japan) na Jesse Were (Zambia) na winga Ayub Timbe (Uchina).

Hata hivyo, Kimanzi atakosa nahodha Victor Wanyama (Uingereza) na beki Joseph Okumu (Uswidi). Olunga, ambaye amekuwa akihangaisha timu katika Ligi ya Daraja ya Pili nchini Japan, ametwikwa majukumu ya nahodha.

Timu hizi zilitoka 1-1 zilipokutana mara ya mwisho mwaka 2017 katika mechi ya kirafiki iliyosakatiwa uwanjani Kenyatta mjini Machakos. Uganda ina rekodi nzuri dhidi ya Kenya ya ushindi 32, sare 22 na vichapo 22 kwa hivyo itaanza mchuano huo na asilimia kubwa ya kurejea jijini Kampala na matokeo mazuri.

Mara ya mwisho Kenya ilichapa Uganda ilikuwa 2-0 mwaka 2015 katika mechi za makundi za soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Cup) jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kikosi kizima cha Uganda

Onyango Denis (Mamelodi Sundowns, Afrika Kusini), Lukwago Charles (KCCA), Odongkara Robert (Horoya, Guinea), Mutakubwa Joel (Kyetume), Willa Paul (Vipers), Kizza Mustafa (KCCA), Ochaya Joseph (TP Mazembe, DR Congo), Awany Timothy (Ashdod, Israel), Juuko Murushid (Wydad Casablanca, Morocco), Revita John (KCCA), Mujuzi Mustafa (Proline), Lwaliwa Halid (Vipers), Kasozi Nicholas ( KCCA), Lwanga Taddeo (Tanta, Misri), Lumala Abdu (Pyramids, Misri), Kizito Luwagga (Shakhter Karagandy, Kazakhstan), Miya Faruku (Konyaspor, Uturuki), Kyambadde Allan (El Gouna, Misri), Kayiwa Allan (Vipers), Aucho Khalid (El Miskir, Misri), Okello Alan (KCCA), Mutyaba Muzamir (KCCA), Okwi Emmanuel (Al Ittihad, Misri), Kaddu Patrick (KCCA) na Bayo Fahad (Vipers).