Uhispania yafunza Ujerumani kusakata gozi la UEFA Nations League
Na MASHIRIKA
KIUNGO mvamizi wa Manchester City, Ferran Torres alifunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya kwanza katika taaluma yake na kusaidia Uhispania kupepeta Ujerumani 6-0 katika UEFA Nations League, Novemba 17, 2020.
Kichapo hicho ndicho kinono zaidi kwa Ujerumani kuwahi kupokezwa katika mashindano ya haiba kubwa. Ushindi huo pia ulirejesha kumbukumbu za fainali ya Euro 2008 ambapo Uhispania waliwazidi nguvu Ujerumani.
Uhispania kwa sasa wanaungana na Ufaransa ambao tayari wamefuzu kwa fainali za Nations League mwaka huu wa 2020. Ubelgiji wa Denmark kutoka Kundi A2 na Uholanzi au Poland kutoka Kundi A1 ndio wwashindani wengine watakaojiunga na wawili hao kwa fainali.
Nyota wa zamani wa Chelsea, Alvaro Morata aliwafungulia Uhispania ukurasa wa mabao kabla ya Torres kufanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 33, sekunde chache kabla ya Rodri kufunga la tatu.
Torres alicheka na nyavu za Ujerumani kwa mara nyingine katika dakika ya 55 na 71 kabla ya Mikel Oyarzabal kufunga la sita mwishoni mwa kipindi cha pili.
Uhispania walimiliki asilimia kubwa ya mpira dhidi ya Ujerumani kuanzia mwanzo hadi mwisho huku wakielekeza jumla ya makombora 23 langoni mwa wapinzani wao.
Ushirikiano mkubwa kati ya Morata na Torres aliyesajiliwa na Man-City kwa kima cha Sh2.8 bilioni muhula huu, ulimtatiza kipa Manuel Neuer.
Kujituma kwa Torres kuliwaaminisha zaidi mashabiki wa Man-City ambao walimshuhudia Leroy Sane ambaye nafasi yake ilijazwa na Torres ugani Etihad baada ya kuhamia Bayern Munich mwishoni mwa msimu jana, akishindwa kabisa kutambisha Ujerumani.
Ujerumani walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi yoyote mwaka huu wa 2020 huku wakidhibiti pia kileleni cha Kundi A4. Masogora hao wa kocha Jaochim Loew walihitaji ushindi dhidi ya Uhispania ili kutinga fainali za Nations League.
Licha ya kujivunia huduma za mafowadi matata Serge Gnabry wa Bayern na sajili mpya wa Chelsea, Timo Werner, Ujerumani ambao kwa sasa ni wa 13 kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), walisalia butu kwenye safu ya mbele huku wakishindwa kuelekeza fataki yoyote langoni mwa Uhispania katika dakika 45 za mwanzo.