Michezo

UJERUMANI KIGEZONI: Germany Machine yalia Uholanzi njama

September 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

BERLIN, Ujerumani

UFUFUO wa timu ya Ujerumani utakabiliwa na mtihani wake wa kwanza bila winga wa Manchester City, Leroy Sane wakati timu hiyo itakapowaalika mahasimu wao wa tangu jadi Uholanzi katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Ulaya (Euro 2020) mjini Hamburg, leo Ijumaa.

Sane ni mmoja wa wachezaji kadhaa nyota wa Ujerumani watakaokosa mchuano huu kutokana na jeraha. Wengine ni Julian Draxler na Thilo Kehrer. Sane, 23, aliumia goti katika mechi ya Community Shield ambayo City ilishinda Liverpool mapema mwezi uliopita.

Winga huyu amechangia pakubwa katika ufufuo wa timu ya Ujerumani tokea ipate masikitiko makuu katika Kombe la Dunia mwaka 2018. Ameifungia mabao matano katika mechi sita zilizopita.

Kati ya mabao hayo, mawili yalikuwa dhidi ya Uholanzi, ambayo Ujerumani imekutana nayo mara tatu tangu Oktoba mwaka jana. Hata hivyo, wachezaji wenza walisisitiza mapema juma hili kuwa watajaza nafasi yake bila tatizo.

“Leroy hubuni nafasi kubwa uwanjani na ni muhimu sana katika timu yetu, lakini tuna wachezaji wakali wa kujaza nafasi yake,” mchezaji wa Borussia Dortmund, Marco Reus alisema Jumatano.

Nafasi ya Sane inatarajiwa kuchukuliwa na mshambuliaji matata wa RB Leipzig, Timo Werner, ambaye anadhamiria kupigania nafasi ya kurejeshwa katika kikosi cha kwanza.

“Jeraha la Leroy linamaanisha kuwa kuna nafasi katika idara ya ushambuliaji. Ninaamini ninaweza kuonyesha makali yangu hapa jinsi nimekuwa nikifanya katika klabu,” alisema Werner, ambaye amepachika mabao matano katika mechi tatu za kwanza za Leipzig msimu huu.

Baada ya kushindwa kupiga Uholanzi mara katika Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya (Uefa Nations League) mwaka jana, ushindi wa Ujerumani wa mabao 3-2 mjini Amsterdam mwezi Machi umeonyesha kufufuka kwa timu hiyo, ambayo imefungua mwanya wa alama sita dhidi ya Uholanzi katika mechi za Kundi C.

Kwa hivyo, ushindi mjini Hamburg utaweka Ujerumani katika nafasi nzuri ya kufuzu, kitu ambacho kitachochea zaidi uhasama baina ya majirani hao.

Uholanzi itaingia mchuano huu ikikaribia katika hatari ya kushuhudia ndoto yake ya kurejea katika dimba hili ikififia.

Ni mjini Hamburg ambako Marco Van Basten alipachika bao lililozamisha Ujerumani Magharibi na kuingiza Uholanzi katika fainali ya mwaka 1988, ambayo walishinda taji lao kubwa la mwisho.

Miaka 31 baadaye, Waholanzi wako na shinikizo baada ya kuambulia alama tatu pekee kutokana na mechi mbili za kwanza.

Wanashikilia nafasi ya tatu katika kundi lao, ambayo atakayemaliza katika nafasi hiyo atatokosa tiketi ya moja kwa moja na hivyo kulazimika kulimana na mpinzani mwingine katika mechi ya muondoano ili kufuzu. Kundi hili linaongozwa na Northern Ireland kwa alama 12, ingawa imesakata mechi mbili zaidi ya Uholanzi.

Katika kikao na wanahabari Jumatatu, kocha Ronald Koeman alipuuzilia mbali kuwa mechi dhidi ya Ujerumani ni ya kufa-kupona.

“Mechi hiyo si muhimu sana. Lazima tupate alama 12 dhidi ya Estonia na Belarus na alama nyingine kutokana na mechi mbili dhidi ya Northern Ireland,” alisema Koeman, ambaye alicheza katika nusu-fainali ya mwaka 1988.

Kwingineko, Nemanja Matic amesema kocha Ole Gunnar Solskjaer atajilaumu mwenyewe ikiwa Manchester United haitawania taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Dakika 22 pekee

Matic, aliyewasili uwanjani Old Trafford kutoka Chelsea mwaka 2017, amechezea United dakika 22 pekee msimu huu baada ya kuingia mechi dhidi ya Southampton kama mchezaji wa akiba. United, ambayo ilishinda ligi mara ya mwisho mwaka 2013, inashikilia nafasi ya nane na iko alama saba nyuma ya viongozi Lverpool.

“Kocha lazima aamue kuchezesha wachezaji wanaoweza kupigania taji na asipopata ushindi, anabeba msalaba pekee yake,” Matic aliambia wanahabari timu yake ya taifa ya Serbia ikijiandaa kuvaana na Ureno katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Bara Ulaya (Euro 2020) itakayosakatwa Jumamosi.

“Nimekuwa katika soka kwa muda mrefu. Nimesakata karibu mechi zote katika klabu nimekuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Ili niweze kucheza, mchezaji mmoja alitiwa kwenye benchi na kukubali ukweli huo, na sasa ni zamu yangu.”

Solskjaer ameamua kutumia Scott McTominay kushirikiana na Paul Pogba katika safu ya kati ya United katika mechi nne za kwanza na, ingawa Matic anaheshimu uamuzi huo, amejawa na ari ya kuthibitishia kocha huyo kutoka Norway kuwa hakufanya uamuzi mzuri.

“Katika mechi mbili za kwanza ama tatu alichagua kikosi bila ya kunijumuisha,” Matic aliongeza. “Najitahidi sana kadri ya uwezo wangu. Tunaheshimu uamuzi wake, ni jukumu langu kumuonyesha kuwa alikosea na kunipatia nafasi ninayostahili kuwa.

“Hakuna tatizo. Nilimueleza kuwa sikubaliani naye, lakini jukumu la kuchagua kikosi ni lake.”

United itaalika uwanjani Old Trafford vijana wa Brendan Rodgers Leicester mnamo Septemba 14 baada ya mechi za mataifa.

Aidha, shujaa wa zamani wa United, Paul Scholes haamini katika uwezo wa vijana wa Solskjaer wa kushindania ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka miwili ijayo.