Michezo

Ujerumani yalaza Uholanzi mechi ya kufuzu Euro

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ARMSTERDAM, UHOLANZI

KOCHA Ronald Koeman wa Uholanzi amesema anajutia kutofanyia kikosi chake mabadiliko muhimu mwishoni mwa kipindi cha pili katika mchuano wa Kundi C wa kufuzu kwa fainali za Euro 2020 uliowakutanisha na Ujerumani jijini Amsterdam wikendi ambayo imeisha.

Bao la dakika za mwisho la Nico Schulz lilihakikisha kwamba vijana wa kocha Joachim Loew wanalipiza kisasi dhidi ya Uholanzi waliowachabanga 2-0 katika mechi ya Nations League mnamo Novemba 2018.

Nico Schulz wa Ujerumani afungia timu yake bao la tatu Ujerumani iliposhinda wenyeji Uholanzi 3-2 Machi 24, 2019, uwanjani Johan Cruyff Arena jijini Amsterdam. Picha/ AFP

“Nilitaka sana kumleta Nathan Ake kujaza nafasi ya QWuincy Promes. Ni mabadiliko ambayo yangetuweka katika nafasi ya kutia kapuni angalau alama moja muhimu,” akasema Koeman katika mahojiano yake na wanahabari mwishoni mwa mechi.

Leroy Sane wa Manchester City aliwafungulia Ujerumani ukurasa wa mabao baada ya kushirikiana vilivyo na Serge Gnabry aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya Matthijs de Ligt.

Ingawa mabao ya De Ligt na Memphis Depay yalisawazisha mambo, Schulz alikiyumbisha kabisa chombo cha wenyeji wao sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa.

Matokeo hayo yana maana kuwa Ireland ya Kaskazini kwa sasa wanaselelea kileleni kwa Kundi C baada ya kuwapepeta Belarus 2-1 ugani Windsor Park. Awali, kikosi hicho kilikuwa kimewachabanga Estonia 2-0 katika mchuano wao wa ufunguzi wa kampeni za kufuzu kwa fainali za Euro mwakani.

Uholanzi ambao pia wamecheza michuano miwili, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu baada ya kuzidiwa maarifa na Ujerumani.

Kujinyanyua

Ujerumani waliokosa huduma za wakongwe Thomas Muller, Jerome Boateng na Mats Hummels ambao kocha Joachim Loew amewatema kabisa, walitumia mchuano dhidi ya Uholanzi kujinyanyua baada ya kubanduliwa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 katika hatua ya makundi.

Licha ya kushindwa, Koeman alikiri kuridhishwa na kuimarika kwa kikosi chake kilichokosa kunogesha fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia mnamo 2018.

Kwingineko, fowadi Eden Hazard wa Chelsea alifunga bao katika mchuano wake wa 100 ndani ya jezi za Ubelgiji na kusaidia kikosi hicho kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Cyprus katika Kundi I.

Hazard aliwaweka Ubelgiji kifua mbele katika dakika ya 10 kabla ya mvamizi Michy Batshuayi kushirikiana vilivyo na Thorgan Hazard ambaye ni kakaye Eden.

Batshuayi ambaye kwa sasa anachezea Crystal Palace amewafungia Ubelgiji jumla ya mabao 13 kutokana na mechi 25 za kimataifa. Scotland walitolewa kijasho kabla ya kuwachabanga San Marino 2-0 huku Urusi wakiwaponda Kazakhstan kwa mabao 4-0.

Ubelgiji ambao walitinga hatua ya nusu-fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka jana, kwa sasa watakuwa wenyeji wa Kazakhstan na Scotland mwezi Juni katika michuano ijayo ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Ratiba ya Leo Jumanne

Kundi J

Armenia na Finland
Bosnia-Herzegovina na Ugiriki
Italia na Liechtenstein

Kundi D
Ireland na Georgia
Uswisi na Denmark

Kundi F
Malta na Uhispania
Norway na Uswidi
Romania na Faroe Islands