Ujio wa Sarri na Emery unawakosesha Klopp na Guardiola usingizi katika EPL
NA CHRIS ADUNGO
MAPEMA wiki iliyopita, kocha Jurgen Klopp wa Liverpool alikiri kwamba mshindi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika kampeni za msimu huu huenda akaamuliwa katika wiki chache za mwisho wa muhula huu.
Na kwa kweli, ligi hiyo inazidi kushika kasi huku utamu zaidi ukinogeshwa na ukubwa wa viwango vya ushindani miongoni mwa klabu zinazofunga orodha ya tano-bora.
Chini ya kocha mpya Maurizio Sarri, ukomavu na umahiri wa masogora wa Chelsea tayari umedhihirisha kwamba wao ni miongoni mwa wagombeaji halisi wa taji la EPL msimu huu.
Ni alama mbili pekee ndizo zinazokitenganisha kikosi hicho na Manchester City na Liverpool wanaodhibiti kilele cha jedwali. Hadi sasa, hizo ndizo timu za pekee ambazo hazijapoteza mechi hata moja.
Nao Liverpool chini ya ukufunzi wa Mjerumani Jurgen Klopp wanazidi kudhihirisha ukubwa wa uwezo walionao katika kuzilipua kambi za wapinzani na washindani wao wakuu.
Matumaini ya Manchester United kunyakua ubingwa wa EPL msimu huu au hata kutinga orodha ya nne-bora yanazidi kufifia kabisa chini ya kocha mzawa wa Ureno, Jose Mourinho. Huu ndio ukweli ambao umewaamshia mashabiki wa kikosi hicho hasira ambazo kwa sasa zinamkosesha Mourinho usingizi.
Chombo cha mabingwa hao wa zamani wa EPL kilizamishwa kabisa na West Ham United wikendi iliyopita kwa kichapo cha 3-1 ugani London.
Licha ya kupoteza mechi mbili za ufunguzi wa msimu huu dhidi ya Man-City na Chelsea, Arsenal wanazidi kurejesha uthabiti wao polepole chini ya kocha mpya Unai Emery. Kikosi hicho kilipata utulivu waliouhitaji zaidi mwishoni mwa wiki jana baada ya kuwapepeta Watford 2-0 uwanjani Emirates.
Pep Guardiola alishinda Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) katika msimu wake wa kwanza akiwa na Barcelona na pia akashinda Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) katika msimu wake wa kwanza akiwa na Bayern Munich. Mkufunzi huyo mzawa wa Uhispania alihitaji misimu miwili nchini Uingereza ili kuwanyanyulia Man-City ubingwa wa EPL muhula jana.
Tangu mwanzoni mwa msimu huu, ufanisi huo wa Guardiola umetosha kuwajengea mashabiki wa Man-City kiota kikubwa cha matumaini kwamba Guardiola atahifadhi ubingwa wa taji la EPL msimu huu.
Na kwa hakika, Man-City wameanza msimu huu vizuri zaidi kwa kutandaza soka safi ambayo imewavunia ushindi mara sita na sare moja katika jumla ya michuano saba iliyopita. Kikosi hicho kwa sasa kinajivunia alama 19 sawa na Liverpool ambao waliwalazimishia Chelsea sare ya 1-1 uwanjani Stamford Brdige wiki jana.
Japo Chelsea wanapigiwa upatu kutawazwa mabingwa wa taji la EPL msimu huu, nina hakika kwamba kuna uwezekano kuwa mshindi wa kombe hilo huenda akajulikana katika wiki za mwisho wakati jamvi la kipute hicho litakuwa likikunjwa rasmi mnamo Mei 2019.
Ingawa Liverpool na Man-City wapo katika nafasi bora zaidi ya kujitwalia ubingwa wa EPL msimu huu kutokana na uthabiti wa vikosi vyao, nahisi kwamba mwamko mpya wa nahodha Eden Hazard pia utawatambisha Chelsea. Tottenham Hotspur ndio wenye uwezo mkubwa wa kuwahini Arsenal nafasi ndani ya mduara wa nne-bora.
Ambacho ni kivutio zaidi, ni viwango vya ushindani miongoni mwa vikosi vinavyowania nafasi nne za kwanza jedwalini huku Guardiola, Klopp, Sarri, Emery, Pochettino na Mourinho wakiendeleza vita vya ubabe.