Michezo

Ukarabati wa uwanja wa Kamariny kukamilika Septemba

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

SHUGHULI za ukarabati katika uwanja wa Kamariny katika eneo la Iten, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet sasa zitakamilika katika kipindi cha miezi minne ijayo.

Haya ni kwa mujibu wa Katibu Msimamizi wa Wizara ya Michezo, Hassan Noor ambaye amesisitiza kwamba serikali imejitolea kuwawekea wanamichezo wa humu nchini miundo-msingi bora katika juhudi za kuikuza sekta ya spoti.

“Kwa sasa tuna hazina ya fedha ya kutegemewa kutoka kwa serikali. Tunatarajia kukamilisha ukarabati wa sehemu iliyosalia ya uga wa Kamariny chini ya kipindi kifupi zaidi kijacho,” akasema Noor.

“Tunafahamu kwamba wanariadha wa Elgeyo-Marakwet ni miongoni mwa wale ambao wamekuwa wakiipeperusha vyema zaidi bendera ya Kenya katika majukwaa ya kimataifa,” akatanguliza.

“Wamefaulu kufanya hivyo licha ya kutokea katika sehemu zisizo na miundo-msingi zozote za kufanikisha maandalizi yao, bila makocha wala akademia za kuwapokeza malezi katika ulingo wa uanariadha,” akasema Noor.

Wakati uo huo, zaidi ya wanariadha 200 na maafisa wa mchezo huo wamenufaika na msaada wa barakoa zinazosambazwa sasa kote nchini na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) katika eneo la Magharibi ya Kenya.

Kati ya wanariadha walionufaika ni wale kutoka katika kaunti za Bungoma, Kakamega, Busia na Vihiga.