Ukosefu wa viwanja vya hadhi unavyoua talanta mitaani
Na SAMMY WAWERU
Rashid Saka ambaye ni mwanasoka chipukizi anayeendelea kupaliliwa makali na timu ya Soccer Wizard, chini ya mwavuli wa Githurai United ni mwingi wa matumaini ipo siku ndoto zake kuchezea timu ya Gor Mahia na Chelsea zitatimia.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 10 ni golikipa hodari aliyetambua kipaji chake katika kandanda akiwa angali mdogo, Kocha Wala akifichua kwamba pia ni straika.
Huku shule na taasisi zote za elimu nchini zikiwa zimefungwa kwa muda kufuatia janga la Covid-19, pamoja na vipaji wengine chipukizi wa Soccer Wizard muda wao mwingi wameuelekeza katika mazoezi.
“Kila siku kuanzia adhuhuri huwa tunafanya mazoezi,” Saka anaelezea. Jumanne, kulingana na Kocha Wala ni siku aliyowatengea, kushirikisha kila mmoja na kuwapa ushauri namna ya kuimarisha talanta. “Jumamosi tunashiriki mechi za kirafiki na timu mbalimbali Githurai na mitaa jirani kama vile Kahawa West, Majengo, Soweto na Kahawa Wendani, miongoni mwa nyinginezo,” Wala anasema.
Jitihada za kocha huyo kunoa vipaji zikipigiwa upatu, ukosefu wa uwanja bora kufanya mazoezi na pia kushiriki michuano ndio kikwazo kikuu.
Pembezoni mwa Shule ya Msingi ya Githurai, Nairobi, ni uga wa kipekee eneo hilo unaotumiwa kufanya mazoezi na kukuza vipaji.
Hata hivyo, hali yake si ya kuridhisha. Umesheheni vumbi, hali ambayo inawatia katika hatari watumizi wake.
“Huu ndio uwanja tunaotumia kupalilia vipaji wetu mtaani humu. Kupata vipaji chipukizi ni hatua, inayoanza wakiwa wangali wadogo kiumri,” Kocha Wala anaeleza, akisema hali ya uga huo imesalia hivyo tangu akiwa mchanga.
“Ni hatari kwa watoto hasa kwa sababu ya magonjwa yanayosababishwa na vumbi,” Kocha huyo analalamika.
Kulingana na Fredrick Ochieng Kocha Msimamizi wa Timu ya Githurai United na All Stars Githurai, jitihada kutaka uwanja huo uimarishwe zimegonga mwamba kwa muda mrefu, kwa kile anataja kama kusababishwa na siasa potovu na utepetevu wa viongozi.
“Tumejaribu kwa muda mrefu kushirikisha viongozi wa eneo hili, wakiwemo madiwani na wabunge wanaochaguliwa kila baada ya miaka mitano kutuimarishia uwanja wa Githurai bila mafanikio. Isitoshe, ombi letu limeingiwa na siasa potovu,” Kocha Ochieng anafafanua, akihofia kizazi kijacho cha wanasoka huenda talanta zao zikakosa kupaliliwa kwa sababu ya hali mbovu ya miundomsingi.
Ni miundomsingi katika kuimarisha sekta ya michezo ambayo pia imepuuzwa katika mitaa mingine Niarobi, Zimmerman ikijumuishwa, huku Shirikisho la Soka Nchini – FKF likionekana kuifumbia macho.
Kwa mfano, katika mtaa wa Zimmerman, vijana waraibu wa michezo hutumia kipande cha ploti kisichozidi ukubwa wa nusu ekari.
Isitoshe, ni ardhi ya mtu binafsi, ambayo wakati ataitwaa kufanya mradi wa maendeleo, watoto na vijana watahangaika kufanya mazoezi.
“Kwa mujibu wa sheria za ujenzi, kila mtaa unapaswa kuwa na nafasi iliyotengewa uga wa umma. Mitaa mingi Nairobi haina, agizo hilo limepuuzwa na ardhi za umma kunyakuliwa,” Charles Njenga, Mwenyekiti wa All Stars Githurai anasema.
Wakati wa mahojiano Kocha Wala aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba hutegemea ufadhili binafsi kuimarisha vipaji wake. “Huwa tunafanya michango kati yetu kununua mipira, majezi na viatu vya mazoezi na kushiriki mechi,” akasema.
Ushirikiano huohuo pia huutumia kuchangisha pesa za kununua unga maalum kuchora mistari ya uwanja, ili kushiriki michuano.
Wakati mwingine hulazimika kukodi uga Ruiru na pia Stima Club Ground, Ruaraka, ili kushiriki mechi, hatua inayowagharimu.
Ni aibu kwa viongozi wa eneo hilo kupuuza ombi la watoto na vijana wenye ari kuimarisha talanta zao katika michezo, ikizingatiwa kuwa miaka ya uchaguzi wakifanya kampeni huwaahidi mbingu na nchi, kupitia maneno matamu ambayo ni ahadi hewa.
Vipaji hao chipukizi ndio mastaa wa kesho, na wanahitaji uwanja ulioimarishwa kwa kupandwa nyasi ikiwa ni pamoja na kupata vifaa muhimu katika kuboresha talanta zao.