Ulikuwa usiku wa sare sare katika robofainali za Uefa
LONDON, Uingereza
Kocha Mikel Arteta amesema makosa madogo madogo kwenye ngome ndio yaliyosababisha kikosi chake cha Arsenal kutoka sare ya 2-2 na Bayern Munich katika mechi muhimu ya robo-fainali ya UEFA, Jumanne usiku.
Kuhusu tukio la penalti ambayo wachezaji wa Arsenal walidai ilikuwa halali baada ya Bukayo Saka kuangushwa na kipa Manuel Neuer mechi ikielekea kumalizika, Arteta alisema mwamuzi, Glenn Nyberg kutoka Sweden alimueleza kilichotokea na akaridhika.
“Aliniambia walichunguza na wakapata Saka alijiangusha wakati kipa alikuwa akienda kuokoa hatari.”
“Ben White alikosa nafasi ya wazi ambayo ingetupa ushindi wa 2-0 kabla ya Bayern kufunga mabao yao. Lakini tutakaa chini na kurekebisha makosa yote yaliyotokea,” aliongeza kocha kiungo huyo wa zamani wa Arsenal.
Katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza iliyochezewa Emirates Stadium, Jumanne usiku, Arsenal walitangulia kupata bao la mapema dakika ya 12 kupitia kwa Bukayo Saka baada ya kuandaliwa na kiungo mahiri, Martin Odegaard.
Katika mechi nyingine ya kiwango cha juu iliyochezewa Santiago Bernabeu, wenyeji Real Madrid walitoka nyuma na kuagana 3-3 na Manchester City mbele ya wengi waliojaa uwanjani humo kwa ajili ya pambano hilo.
Bayern walisawazisha dakika sita baadaye kupitia kwa Serge Gnabry aliyefunga dakika ya 18 kabla ya Harry Kane kuongeza la pili dakika ya 32 kupitia kwa mkwaju wa penalti, baada ya Leroy Sane kuangushwa na William Saliba kwenye eneo la hatari.
Arsenal ambao wamelalamika kunyimwa penalti mechi hiyo ikielekea kumalizika, walipata bao la pili kupitia kwa kiungo mshambuliaji Leandro Trossard dakika ya 78. Raia huyo wa Ubelgiji alifunga bao hilo baada ya kushirikiana na Gabriel Jesus.
Saka alionekana kuangushwa
Baada ya mambo kuwa 2-2 zikibakia dakika 14 mechi kumalizika, timu zote zilifanya mashambulizi ya kutafuta bao la ushindi, lakini hazikufua dafu.
Saka alionekana kuangushwa na kipa Manuel Neuer kwenye kisanduku cha hatari lakini mwamuzi Nyberg alipuuza maombi ya rufaa.
Bayern ambao hawakuwa na mashabiki kutokana na marufuku ya UEFA, wataalika Arsenal katika mechi ya marudiano itakayochezewa Allianz Arena, Jumatano, wiki ijayo.
Uwanjani Santiago Bernabeu nchini Uhispania kati ya Real Madrid na mabingwa watetezi Manchester City, ufundi na ushindani ulikuwa wa kiwango cha juu, ambapo mashabiki walishuhudia mabao matatu yakifungwa katika muda wa dakika 14.
City walitangulia kuona lango la wenyeji mapema dakika ya pili kupitia kwa bao la Bernardo Silva, huku mengine yakipatikana kupitia kwa Phil Foden na Josko Gvardiol, dakika za 66 na 71 mtawalia.
Ruben Dias wa Manchester City alifunga langoni mwake katika juhudi za kujaribu kuokoa hatari na kupatia wenyeji bao la kwanza, kabla ya mengine kumiminwa wavuni na Rodrygo dakika ya 14 na Federico Valverde 76.
“Tumetoka sare nyumbani, lakini tunatarajia kucheza vizuri zaidi katika mkondo wa pili, tukilenga ushindi ili tusonge mbele,” alisema kocha Carlo Ancelotti wa Real Madrid.