Ulinzi na Sofapaka zatupwa nje ya SportPesa Shield
Na GEOFFREY ANENE
KLABU za Ulinzi Stars na Sofapaka kutoka Ligi Kuu zimeaga mashindano ya soka ya SportPesa Shield baada ya kuchapwa na wanyonge SS Asad na Bungoma Superstars, huku Kariobangi Sharks, AFC Leopards, Western Stima na Bandari wakisonga mbele, Jumamosi.
Wanajeshi wa Ulinzi pamoja na Sofapaka almaarufu Batoto ba Mungu wote walipoteza mechi zao za raundi ya 32-bora kupitia mikwaju ya penalti.
Baada ya kulazimishiwa sare ya 0-0 katika muda wa kawaida, Ulinzi ililemewa na Assad 5-4 kwa njia ya penalti. Sofapaka, ambayo ililimwa 3-2 na Sharks katika fainali ya mwaka 2018, ilipata dozi sawa na ya Ulinzi. Ilikuwa imekabwa 0-0 dhidi ya Bungoma Superstars kabla ya kuzidiwa maarifa katika upigaji wa penalti.
Sharks pamoja na mabingwa wa mwaka 2017 Leopards na mwaka 2015 Bandari wote walivuna ushindi katika muda wa kawaida. Timu ya Sharks ilipepeta Elim 5-0 uwanjani Bukhungu mjini Kakamega, Leopards ikazima Transfoc kutoka Kitale 4-0 uwanjani humu nayo Bandari ikafunga Kayo bao moja chungu uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi.
Matokeo ya raundi ya 32-bora ya Machi 16, 2019:
Uprising 0-5 Western Stima (Ruaraka Grounds)
Congo Boys 2(3)-2(2) Kenya Police (Serani Sports Grounds)
SS Assad 0(5)-0(4) Ulinzi Stars (Ukunda Show Grounds)
Bungoma Superstars 0(5)-0(4) Sofapaka (Sudi Stadium)
Murang’a Seal 4-1 Kisumu All Stars (Kiharu Stadium)
Dero 2-0 FC Talanta (Moi Stadium Kisumu)
Sindo United 0-1 KCB (Moi Stadium Kisumu)
Vihiga Sportif 2-0 Ushuru (Mumias Sports Complex)
Elim 0-5 Kariobangi Sharks (Bukhungu Stadium)
Transfoc 0-4 AFC Leopards (Bukhungu Stadium)
Kayo 0-1 Bandari (Camp Toyoyo)
Transmara Sugar vs Bidco United (Gusii Stadium)